Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Klopp amkataa Belligham, ageukia wakali hawa

Jude Belligham Bvb Jude Belligham

Sat, 15 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Liverpool imesitisha mpango wake wa kunasa saini ya kiungo wa Borussia Dortmund, Jude Bellingham dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya, imeelezwa.

Staa huyo wa kimataifa wa England, Bellingham amekuwa akihusishwa na mpango wa kubadili timu wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa na kuna timu kibao za Ligi Kuu England zimekuwa zikitajwa kuhitaji huduma yake.

Inaelezwa Dortmund wapo tayari kumuuza kiungo huyo, lakini bei yake inatajwa ni Pauni 130 milioni, jambo ambalo Liverpool wanadhani ni kubwa sana na hawapo tayari kulipa kusajili mchezaji mmoja kwa gharama hiyo.

Kutokana na hilo, Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp sasa atakuwa na machaguo mengine kibao ya viungo ambao anaweza kuwasajili kwenye dirisha lijalo tena kwa gharama nafuu ili wakakipige Anfield.

Moises Caicedo

Kiungo Moises Caicedo bila shaka atahitaji kwenda kujiunga na timu itakayompa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na amekuwa akihusishwa na vinara wa Ligi Kuu England, Arsenal. Arsenal ilijaribu kumsajili Januari, lakini ikashindwa. Liverpool wana nafasi ya kwenda kunasa saini yake kwenye dirisha lijalo na anauzwa zaidi ya Pauni 80 milioni.

Alexis Mac Allister

Alexis Mac Allister alifanya kweli kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, alikokuwa na kikosi cha Argentina. Kiungo huyo anatamba Ligi Kuu England kwenye kikosi cha Brighton. Shida inayowakabili Liverpool kwenye mpango wa kumsajili Mac Allister ni kama watashindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya. Staa huyo anasakwa pia na Manchester United.

Mason Mount

Kinachonekana ni Mason Mount ataachana na Chelsea mwisho mwa msimu huu. Huu ni mwaka wake wa mwisho wa mkataba na hakuna dili jipya lililosainiwa hadi sasa. Newcastle United wanahitaji saini yake, lakini Liverpool watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kunasa huduma yake kama watakuwa siriazi kwenye mpango wa kumsajili. Mount atatua Anfield.

Matheus Nunes

Licha ya msimu wake wa kwanza kuwa wenye kupanda na kushuka huko Wolves, Matheus Nunes amekuwa akiwavutia sana Liverpool. Mapema mwaka huu kulikuwa na ripoti kwamba kuna makubaliano ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 kwenda kukipiga Anfield mwisho wa msimu. Hilo linathibitisha kwamba Liverpool wanamtaka staa huyo anayeuzwa Pauni 50 milioni.

Declan Rice

Declan Rice ni kama Bellingham tu, amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na klabu kubwa zaidi. Kiungo huyo wa West Ham, jina lake limekuwa likihusishwa na vigogo kama Manchester United, Manchester City, Chelsea, Arsenal na sasa Liverpool. Hata hivyo, huduma ya Rice nayo itakuwa gharama kubwa, West Ham United wanataka Pauni 100 milioni.

Nicolo Barella

Katika umri wa miaka 26, kiungo Nicolo Barella yupo kwenye kiwango bora kabisa cha soka lake na ameripotiwa huduma yake inaweza kupatikana kwa Pauni 60 milioni tu. Shida inayowakabili Liverpool kwenye mchakato wa kumpata staa huyo ni kama watafeli kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Barella huenda akagomea ofa yao.

Joao Palhinha

Moja ya wachezaji wasiopewa sifa zao wanazostahili huko Fulham kutokana na anachofanya kwenye Ligi Kuu England. Palhinha anafahamika vyema na idara ya skauti ya klabu ya Liverpool na hakika saini yake iligharimu Pauni 20 milioni tu aliposajiliwa kutoka Sporting CP mwaka jana. Anamudu zaidi kiungo ya kukaba kuliko kushambulia, lakini umri wake miaka 28.

Teun Koopmeiners

Teun Koopmeiners umri wake ni miaka 24, lakini ameonyesha ukomavu mkubwa ndani ya uwanja kutokana na kile ambacho alifanya AZ Alkmaar, Atalanta na timu ya taifa ya Uholanzi. Teun anaweza kucheza kiungo ya chini au ya juu, hata hivyo huduma yake haiwezi kuwa rahisi kwa sababu ni mmoja wa wachezaji muhimu sana huko Bergamo.

Adrien Rabiot

Jina la staa mkubwa kabisa kwenye soka ambaye amekuwa akihusishwa na mpango wa kutua kwenye Ligi Kuu England. Kiungo Adrien Rabiot mkataba wake huko Juventus utafika tamati mwisho wa msimu huu, licha ya timu hiyo ya Serie A kupanga kumwongezea dili jipya. Umri wake bado unaruhusu na Liverpool watakuwa wamepata mtu wa maana wakimsajili.

Sofyan Amrabat

Tangu alipoonyeshwa kiwango bora kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 alikokuwa na kikosi cha Morocco, Sofyan Amrabat amekuwa akihusishwa na Liverpool. Kwa sasa kiungo huyo anakipiga Fiorentina ya Serie A. Uhodari wake kwenye kiungo ya kukaba ndio unaofanya asakwe na timu nyingi na bila ya shaka Liverpool itakuwa kwenye mikono salama ikimnasa staa huyo.

Manu Kone

Manu Kone anacheza soka lake huko Bundesliga kwenye kikosi cha Borussia Monchengladbach. Kuna wakati alihusishwa sana na Newcastle United, lakini katika kupata wachezaji mahiri na wenye huduma safi uwanjani, Liverpool inaweza kuchangamkia fursa hiyo. Mfaransa huyo ana umri wa miaka 21 na huduma yake inaweza kupatikana kwa Pauni 30 milioni tu.

Luka Sucic

Luka Sucic ni jina ambalo Liverpool wamekuwa wakilifuatilia kwa muda mrefu na bila ya shaka ni miongoni mwa mastaa wanaoweza kutua Anfield kwenye dirisha lijalo. Staa huyo amekuwa na mafanikio makubwa Red Bull Salzburg na hilo linaweza kuwashawishi Liverpool kwenda kunasa siani ya kinda huyo mwenye umri wa miaka 20. Anatengeneza na kufunga mabao pia.

Ryan Gravenberch

Ryan Gravenherch ni mmoja wa wachezaji mahiri kabisa ambao watakuwa sokoni kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi huko Ulaya. Maisha yake yamekuwa magumu huko Bayern Munich tangu alipojiunga akitokea Ajax mwaka jana. Liverpool ilikaribia kumnasa kabla hajaenda Munich na sasa wanaweza kurudi kusaka upya saini ya kinda huyo mwenye miaka 20.

Gavi

Hali ya mambo ya kiungo Gavi haieleweki huko Barcelona baada ya timu hiyo kukabiliwa na ukata uliowafanya washindwe kumworodhesha kwenye kikosi chao cha kwanza. Kutokana na hilo, kocha Klopp anaweza kushangamkia fursa hiyo ya kwenda kunasa saini ya Gavi kama ikionekana Barca bado wapo kwenye hali mbaya ya kiungo. Hata hivyo, saini yake itaibua vita kali.

Conor Gallagher

Kiungo, Conor Gallagher amekuwa akihusishwa na mpango wa kuachana na maisha ya Stamford Bridge. Kwenye dirisha la Januari aliwindwa sana na timu za Everton na Crystal Palace, huku Newcastle United ikipanga kusaka saini yake kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Lakini, Liverpool inaweza kutumia fursa ya kunasa staa huyo akatua Anfield.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live