Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Klabu zijaribu kuepuka aibu hii

Singida X Gyan Klabu zijaribu kuepuka aibu hii

Thu, 16 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tumesema na tunarudia kuzikumbush klabu kuheshimu mikataba zinayoingia na wachezaji au makocha, kwani imekuwa ikizitia aibu.

Kila mmoja anajua mkataba ni mafungamano ya pande mbili katika makubaliano ya jambo fulani, hivyo kila mmoja huwa na wajibu wa kutekeleza kwa ufanisi na pale unapokiukwa moja kwa moja huvunjika na pande iliyosababisha hubeba jukumu la kulipa fidia.

Katika soka la kisasa mikataba imekuwa ikitawala katika usajili wa wachezaji na makocha ambapo pande mbili hulazimika kulinda na kuutekeleza hadi kipindi cha muda waliowekeana. Mara kadhaa katika soka la mataifa yaliyoendelea imekuwa ikishuhudiwa klabu zikiingia gharama kubwa pale zinapovunja mikataba yao ama na wachezaji au wachezaji. Ni mara chache kushuhudia wachezaji wakilazimika kulipa fidia klabu kwa kuvunja mkataba sababu mara nyingi huwa wepesi kuutumikia kwa ufanisi hadi klabu zinapoona hawana faida nao uamua kuvunja mikataba.

Hivi majuzi Singida Big Stars imejikuta ikizuiwa kusajili kutokana na kesi iliyofunguliwa na nyota kutoka Ghana, Nicholas Gyan, ikiwa ni siku chache tangu Tabora United nayo kuingia matatani kwa kushtakiwa Shirikisho la Kimataifa y Soka (Fifa). Klabu kongwe za Simba na Yanga mara kadhaa zimejikuta zikiingia matatani kutoka kwa makocha na mastaa waliowavunjia mikataba kisha kushindwa kuwalipa kwa wakati gharama za fidia ya kuvunjwa.

Ni mara chache kusikia mchezaji akitaka kuvunja mkataba kama alivyowahi kufanya Elias Maguri alipoachana na Simba misimu kadhaa iliyopita au hivi karibuni, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyekuwa akitaka kuitema Yanga ili ajiunge na Azam FC. Hata hivyo, pamoja na kwamba mikataba huvunjwa kwa lazima kutegemea na mazingira yaliyopo, lakini kwa muda mrefu kumekuwa na sintofahamu baina ya pande mbili kwa maana ya viongozi wa klabu na wachezaji ama makocha katika utekelezaji wa mikataba wanaoingia mapema kwa makubaliano ya kufanya kazi.

Wachezaji ama kwa kutotambua mikataba inasema nini au kwa jeuri wamekuwa wakikiuka baadhi ya vipengele na kuingia matatani na viongozi, kadhalika viongozi ama klabu zimekuwa zikishindwa kutekeleza mikataba yao na wachezaji na kusababisha sintofahamu kama iliyowahi kujitokeza siku za nyuma na hata sasa pale Yanga.

Kama pande zilizoingia mkataba zimeshindwa kulinda na kuendelea na mikataba ni bora kuachana kwa kufuata sheria na taratibu kuliko hali ya kutibuana na kusababisha kuzusha uhasama na hata kufikishana mbele ya mashirikisho ya soka nchini (TFF) ama lile la Afrika (CAF) na lile la kimataifa (Fifa) ili kushinikizana kulipana fidia ya kuvunjiana mikataba. Hii ni aibu.

Hata katika ndoa hutokea wanandoa wakashindwana na njia rahisi ya kuachana ni kupeana talaka bila kuumizana ilihali wawili hao walipendana kwa hiari. Ndio maana tunasisitiza kuwa klabu na wachezaji na hata makocha kila mmoja kubeba jukumu la kulinda na kutekeleza kwa umakini, uadilifu na uaminifu mikataba wanayoingia pamoja ili kuepuka sintofahamu.

Chanzo: Mwanaspoti