Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Klabu zavalia njuga corona

99511 Klabu+pic Klabu zavalia njuga corona

Fri, 20 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Klabu za soka zimeonyesha mwitikio wa haraka agizo lililotolewa na Serikali la kusimamisha shughuli za michezo na mashindano ya soka nchini.

Serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa juzi ilitangaza hatua mbalimbali za kuchukua kuepuka kasi ya maambukizi ya virusi vya corona ambavyo hadi sasa watu watatu wamebainika kuathirika navyo nchini.

Miongoni mwa hatua hizo ni kusitisha mikusanyiko ya watu, pia kusimamisha mashindano yote ya michezo kwa mwezi mmoja yakiwemo Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Kombe la Azam Sports Federation.

Kana kwamba haitoshi, muda mfupi baada ya agizo la Serikali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kusimamisha mashindano yote nchini kwa siku 30 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu.

Ikiwa ni siku moja tu tangu uamuzi huo uchukuliwe, klabu za soka nchini zimetangaza kuunga mkono uamuzi huo kwa kuchukua hatua kadhaa za kuhakikisha haziathiriki na kasi ya ueneaji wa virusi hivyo huku zikitangaza kuunga mkono kampeni ya kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Idadi kubwa ya klabu hizo zimetoa mapumziko kwa wachezaji wake na kutangaza mikakati ya kuwalinda wachezaji, familia zao na hata mashabiki juu ya tatizo hilo.

Pia Soma

Advertisement
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Namungo, Hassan Zidadu alisema wachezaji wa timu hiyo wamepewa mapumziko mafupi wakati huu ambao klabu inajipanga kuchukua hatua stahiki za kuwalinda.

“Tumepokea agizo la Serikali nA taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) la kusimamisha kwa muda ligi na mashindano yote ya soka.

Kwa upande wetu tumetoa likizo ya siku 10 kwa wachezaji wetu na baada ya hapo watarejea kambini,” alisema Zidadu.

Kwa mujibu wa Zidadu, uongozi umeahidi kushiriki kikamilifu kutoa elimu kwa jamii namna ya kuepuka na kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.

“Tumewaasa wachezaji wetu wawe makini na wafuate taratibu na kanuni zinazotakiwa ili kuepuka maambukizi ya corona vilevile tunaiweka kambi katika hali ya usafi na tahadhari zote.

“Watakaporudi watachukuliwa vipimo wote ili kujiridhisha kuwa hawajapata maambukizi,” alisema Zidadu.

Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Massau Bwire alisema kuwa wachezaji wao wamepewa ruhusa ya siku 18 iliyoambatana na elimu juu ya janga hilo.

“Tulikaa kikao cha dharura na kuamua kuvunja kambi hivyo wachezaji wetu wanatarajiwa kurejea kambini Aprili 6 lakini itategemea na hali itakavyokuwa kwa wakati huo.

“Tumewalipa tangu tarehe 16 hakuna mchezaji ambaye ameondoka akiwa mnyonge,”alisema Bwire.

Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema kuwa wamechukua tahadhari ya kuwalinda wachezaji wao.

“Tumechukua tahadhari, madaktari wapo, maji yapo ya kutosha kwenye kambi zao wamepewa elimu tutakuwa tunaendelea na mazoezi kama kawaida baada ya mapumziko ya hizo siku tatu,” alisisitiza Kimbe.

Uongozi wa Simba kupitia kwa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa umetangaza kuitisha kikao cha kujadili suala hilo ambalo limezua taharuki duniani.

“Muda sio mrefu nitakuwa na kikao na viongozi wa timu zote za Simba kuweza kuzungumza nao na tutatoa taarifa rasmi lakini tutambue kuwa huu ugonjwa ni hatari.

“Sio ugonjwa wa masihara ni lazima tuchukue tahadhari katika hili. Kama kutasimamishwa programu za wachezaji watapewa utaratibu wa kufanya mazoezi watakapokuwa nyumbani,”alisema.

Klabu hizo pia zimekuwa zikitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kutoa elimu juu ya mbinu za kujikinga na maambukizi ya homa ya corona.

Hata hivyo wakati kundi kubwa la klabu likitangaza kutoa mapumziko kwa wachezaji wao, Gwambina inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza imesema haitavunja kambi.

“Tulikuwa na kikao cha viongozi na maazimio yetu ni kutovunja kambi moja kwa moja na ikibidi tutatoa ruhusa kwa wachezaji wa karibu kuondoka lakini tulichofikiria haraka ni kuzuia muingiliano na hadi sasa tunaamini wachezaji wetu wako salama,” alisema Katibu Mkuu wa Gwambina, Daniel Kirai.

Imeandikwa na Saddam Sadick, Clezencia Tryphone, Eliya Solomon na Charles Abel

Chanzo: mwananchi.co.tz