Mchezaji wa zamani wa CDA, Reli na Kagera Sugar, Selemani Msagasumu amekunwa na uwezo unaooneshwa na winga wa Singida Big Stars, Nickson Kibabage huku akimtabiria makubwa zaidi.
Kibabage alionesha uwezo mkubwa katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Mbeya City kwa kutengeneza mabao mawili (assist) yaliyofungwa na Bright Adjei na Francy Kazadi.
Mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, KMC na Difaa Al Jadid ya nchini Morocco pia humudu kucheza nafasi ya beki wa kushoto.
Msagasumu alisema tangu Kocha Hans Plujm amtumie nafasi ya winga amekuwa akionesha uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga.
“Nilimuona katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Dodoma Jiji alifunga na kutengeneza bao yule ni mchezaji anajua sana mpira na naamini atafika mbali,”alisema mshambuliaji huyo wa zamani ambaye amewahi kuichezea Simba.