Beki wa Simba, Henock Inonga ‘Varane’ aliesajiliwa hivi karibuni kwa mabingwa hao wa nchi anaonekana kuleta upinzani mkubwa katika eneo la beki wa kati ambapo kulikuwa kumetawaliwa na pacha ya Paschal Wawa na Mkenya Joasha Onyango.
Inonga ambae alipata nafasi katika mchezo wa kwanza Ligi ya Mabingwa dhidi ya Jwaneng Galaxy FC ya Botswana atampa wakati mgumu mkongwe, Joash Onyango kurudi kikosini kwani alichokifanya katika mchezo huo hakuna alieona pengo la Onyango.
Miongoni mwa sifa anazomwagiwa Inonga, ni beki mzuri, mtulivu akiwa na mpira anatoa pasi zinazofika anajua kucheza na mpira na anatumia akili kucheza na sio nguvu kama mabeki wengi walivyozoeleka.
Inonga pia anasifika kuwa na vitu vya ziada ambavyo ni nadra kuvikuta kwa mabeki wa Simba waliopo ikiwemo kurukia mipira ya juu na anaonekana ni mtu mwenye kasi.
Simba itashuka dimbani mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Jwaneng Galaxy kutoka nchini Botswana kwenye mchezo wa kuwania kufuzu kwa hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.