Afisa Habari wa Klabu ya Geita Gold FC Hemed Kivuyo ameonesha kusikitishwa na hatua ya kikosi chao kupangiwa kukutana na Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ Young Africans katika mchezo wa Robo Fainali.
TFF kwa kushirikiana na Wadhamini wakuu wa ‘ASFC’ Azam Media juzi Jumatano (Machi 15) walichezesha Droo ya Robo Fainali na miamba hiyo kukutana tena, ikiwa ni siku chache baada ya kukutana katika mchezo wa Ligi Kuu na Geita Gold FC kukubali kichapo cha 3-1.
Baada ya mchezo huo wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam, Kivuyo alisema anatamani kuona timu yao inakutana na Young Afrika katika Hatua ya Robo Fainali ya ASFC, ili kulipa kisasi.
Hata hivyo Kivuyo ametoa sababu za kusema hivyo baada ya kupangwa kwa Droo ya Robo Fainali ya ASFC, ambapo amesema aliomba kukutana na Young Africans akiamini huenda wamepangiwa kucheza katika Uwanja wao wa nyumbani, ila kwa namna ambavyo Droo imeonyesha ni wazi kuwa hawatakuwa na nafasi kubwa ya ushindi ugenini.
“Kiukweli nilitamani kukutana na Young Africans ila katika Uwanja wa nyumbani na si ugenini, kwani tunaimani nyumbani tuna Mashabiki wengi ambao wangetupa nguvu ya kuwafunga Young Africans na kisha kuingia Nusu Fainali, ila kwa namna ilivyochezeshwa Droo hatuna matumaini makubwa ya kushinda ugenini tena,” amesema Kivuyo.
Young Africans na Geita Gold FC zote zilishafuzu kucheza hatua ya Robo Fainali ya Kombe la (ASFC) baada ya kuwafunga Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 3-1, huku Geita wakiwachapa Green Warriors mabao 3-1.
Michezo mingine ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ ambayo imepangwa kuchezwa mapema mwezi Aprili.