Licha ya chama lake, Zulte Waregem kushuka daraja huko Ubelgiji, kiungo wa Kimataifa wa Tanzania, Novatus Dismas ameziingiza vitani Southampton na Middlesbrough za England kupigania saini yake.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na timu hiyo msimu uliopita wa kiangazi akitokea Israel ambako alikuwa akiichezea Maccabi Tel Aviv na kuwashangaza wengi kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi.
Akiwa na Zulte Waregem, Novatus ametumika kama beki wa kati, kushoto, winga na muda mwingine alicheza kama kiungo mkabaji nafasi ambayo Watanzania wengi wamezoea kumwona akicheza tangu akiwa kwa mkopo Biashara United ya Mara.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, Southampton iliyoshiriki Ligi Kuu England (EPL) msimu uliopita kabla ya kushuka Daraja ndio klabu inayoongoza vita hiyo huku wakifuatiwa kwa karibu na Middlesbrough ya Daraja la Kwanza 'EFL Championship' na wapo tayari kutoa Euro 550k (Sh 1.3bilioni).
Ikumbukwe ya kuwa Southampton ni miongoni mwa klabu za daraja la kati England ambazo zimekuwa zikilea na kuibua wachezaji wengi ambao wamekuwa wakifanya makubwa kwenye Ligi ya England mfano mzuri ni Sadio Mane ambaye alitamba akiwa na Liverpool kabla ya kwenda Bayern Munich, Virgil van Dijk.
Wengine ni Luke Shaw, Morgan Schneiderlin, Adam Lallana, Danny Ings, Dejan Lovren, Calum Chambers, Nathaniel Clyne, Jannik Vestergaard, Pierre-Emile Hojbjerg, Matt Targett, Graziano Pelle, Gareth Bale, Victor Wanyama, Oxlade-Chamberlain, Dusan Tadic, Jay RodrÃguez.
Taarifa kutoka Ubelgiji, zinasema Zulte Waregem wanaweza kumwachia Novatus na winga wa Gambia Alieu Fadera ambaye anahusishwa na Manchester United katika dirisha hili la usajili ili kupata fedha ambazo zitawafanya kukiboresha kikosi chao kwa ajili ya kuanza maisha mapya ya Ligi Daraja la Kwanza Ubelgiji. Novatus alicheza mechi 36 akiwa na Zulte Waregem msimu huu.
Hakufunga bao lolote lakini alitoa pasi mbili za mabao. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 ni mchezaji wa timu ya taifa 'Taifa Stars' na ameifungia mabao mawili.