Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiungo mpya Simba aitingisha Yanga SC

Okejepha Simba.jpeg Kiungo mpya Simba aitingisha Yanga SC

Tue, 23 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo mpya wa Simba, Augustine Okejepha, amefungukia mipango mikali aliyonayo msimu ujao, akieleza namna makocha wanavyokoleza moto kambini, huku akituma salamu Yanga akisema “subirini muone.”

Okejepha amesajiliwa na Simba hivi karibuni akitokea Rivers United ya Nigeria, ambapo msimu uliopita alikuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu nchini humo.

Nyota huyo ambaye ni kiungo mkabaji aliyetua Simba baada ya kuondoka kwa Sadio Kanoute na Babacar Sarr, hivi sasa yupo Misri na kikosi cha timu hiyo kilichoweka kambi kujiandaa na msimu mpya katika Mji wa Ismailia.

Kuhusu Yanga

Mnigeria huyo amesema taarifa za Yanga anazo na kilichopo sasa ni shauku yake kukutana na timu hiyo uwanjani ili kuonyeshana ubabe kwani anataka kuendeleza rekodi yake ya msimu uliopita.

“Yanga wamebeba ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu, sasa ni zamu yetu na hilo tutakwenda kudhihirisha msimu ujao kwani tumejipanga vizuri hivyo tutacheza nao tukiwa sawa kinguvu, kiakili na kimbinu, hakuna kitakacho tushinda, subirini muone,” alisema.

Kiungo huyo alisema kwamba ujio wake ya Simba ni mpango maalumu wa viongozi baada ya msimu uliopita timu hiyo kutokuwa na matokeo mazuri uwanjani.

“Nimeletwa Simba ili kutuliza presha ya mashabiki, wapinzani wetu nawajua vizuri na mwisho wao umekaribia kwani ninaamini kupitia wachezaji wenzangu waliobora tutakwenda kujenga timu ya tofauti ambayo haijawahi kutokea ndani ya Tanzania na itaongoza tena,” alisema Okejepha.

Msimu ujao sasa

Aidha aliweka wazi kuwa msimu ujao hautakuwa rahisi kwani ana uzoefu wa kutosha kuhusu michuano ya kimataifa hivyo hakuna kitakachoharibika kwani tayari alishajipanga kuja kupambana zaidi ya msimu uliopita huko alipokuwa.

“Msimu ujao hautakuwa mwepesi kwani tumejipanga sana hivyo ushindi ni lazima kwani wachezaji waliopo ndani ya kikosi chetu wana ubora na uzoefu na michuano ya kimataifa hivyo hakuna jambo gumu zaidi ya kuongeza juhudi.

“Naifahamu Simba ni timu kubwa na mashabiki wanachotaka ni matokeo mazuri kwenye ligi na kimataifa. Makocha tulionao ni wenye ubora mkubwa hivyo msimu ujao watarajie rekodi za watu kuvunjwa na makombe kubebwa na sisi,” alisema.

Okejepha katika nafasi anayocheza Simba yuko pamoja na mastaa wenzake wapya ambao ni Yusuf Kagoma kutoka Singida Black Stars na Debora Fernandes aliyetokea Mtondo ya Zambia. Pia yupo Mzamiru Yassin na Fabrice Ngoma waliokuwepo tangu msimu uliopita.

Uwepo wa nyota hao watano eneo la kiungo mkabajji ni wazi kutakuwa na ushindani mkubwa wa namba hivyo yule atakayeonyesha kiwango bora ndiye atapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza chini ya Kocha Mkuu mpya, Fadlu Davids.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live