Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiungo fundi asiyeisahau Yanga, Sure Boy amjaza upepo

Balama Mapinduzi Mapinduzi Balama

Tue, 1 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu wa 2019 Yanga iliinasa saini ya Balama Mapinduzi ‘Kipenseli’ wa Alliance kwa mkataba wa miaka mitatu.

Mwanaspoti limepata nafasi ya kufanya mahojiano na kiungo huyo fundi ambaye amerudi tena uwanjani akiitumikia Mtibwa Sugar na kufunguka mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuweka wazi sababu ya mastaa wazawa kushindwa kufanya vizuri wakitua Simba na Yanga.

“Hakuna ambaye hapendi mafanikio ndani ya timu hizo shida ni kutokuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara kama ilivyokuwa tulikotoka lakini uwezo wa kufanya hivyo tunao,”

VIUNGO HAWA

Kipenseli anasema hakuna raha kama kumwangalia kiungo anayecheza mpira akipokea anautoa, huo ndio utamaduni wake na asilimia kubwa amekuwa muumini wa mastaa wanaocheza nafasi hiyo ambao wanapokea na kutoa.

“Hata ukiwafuatilia mastaa wengi wanaonivutia utagundua nawapenda kwasababu ni watu wa wanaopokea na kuachia ni vigumu mchezaji wa aina hiyo kuumia kwasababu hawaguswi sana na wapinzani.

“Sijisifii ila naamini katika kipaji na nimekuwa na utaratibu wa kurudia mechi ambazo nimecheza na kubaini nakuwa bora zaidi nikicheza namba nane japo nafasi nyingine zote ninazopewa kucheza nafanya vizuri.”

MWALYANZI, FEI TOTO BALAA

“Kuna viungo wengi nimebahatika kukutana nao na wengine nimecheza nao timu moja lakini hawa watatu nawakubali sana na wana uwezo mkubwa wa kucheza.

“Feisal Salum ‘Fei Toto’, Salum Aboubkary ‘Sure Boy’ na Peter Mwalyanzi ni mafundi wa mpira ambao nikikutana nao huwa najiandaa tofauti na ninapokutana na wapinzani wengine hii ni kwa sababu tunafahamiana, unajua mchezaji fulani anachezaje na najiandaa namna ya kumkaba.”

Kipenseli anasema kuna kazi ya kufanya kuwakaba viungo hao na anakumbuka akiwa Alliance dhidi ya Kagera Sugar alikutana na Mwalyanzi na alimpa tabu.

ISINGEKUWA YANGA

“Nilisajiliwa na Yanga nikitokea Alliance nimeitumikia timu hiyo msimu mmoja na kuuguza majeraha misimu miwili mfululizo, haikuwa rahisi kwangu. Nawashukuru viongozi wa timu hiyo kwa kunijali na kipindi chote nilipokuwa na matatizo,” anasema na kuongeza;

“Ni gharama kubwa imetumika hadi kufikia hapa nilipo, kama Yanga wangeamua kunitupa basi maisha yangu ya soka yangeishia hapo. Nisingeweza kumudu gharama. Nimetibiwa ndani na nje ya nchi ndio hali yangu imetengamaa hadi sasa nacheza.”

Kipenseli anasema hajutii misimu miwili bila kucheza kwasababu kilichotokea ni mipango ya Mungu na ingekuwa ni mipango yake, basi asingeruhusu hilo litokee ili aweze kuitumikia Yanga kwa misimu yote.

“Kuna wakati wa Mungu na wakati tunaopanga sisi, hayo yalitokea niliyapokea kama changamoto sasa namshukuru Mungu nimerudi tena uwanjani naamini ndoto yangu itatimia nitapambana hadi mwisho ili kuweza kufikia malengo.”

SURE BOY AMJAZA UPEPO

Ndoto inaishi ndio anavyosema Kipenseli baada kuendelea kukipiga Ligi Kuu kuthibitisha ndoto yake tangu akiwa mdogo ilikuwa ni kucheza kwa mafanikiwa kupitia miguu yake.

“Napenda mpira naishi mpira kwenye familia yetu wakubwa zangu wote walipenda soka. Naamini ndoto yangu ilikuwa ni soka kwani mambo ya shule nilikuwa sizingatii sana kama na ndio maana nakipiga hadi sasa,” anasema na kuongeza;

“Mbali na kuvutiwa kaka zangu ambao ndio walionipeleka kwenye viwanja vya mazoezi nikianza kwa kuwabebea viatu nilikuwa navutiwa zaidi na uchezaji wa Sure Boy ambaye ndiye amenifanya nikipige Ligi Kuu.

“Ukiniambia nikutajie wachezaji watatu walionifanya nisikosekane kiwanjani na kuwa mtoro darasani nitarudia jina la Sure Boy mara tatu.

KUISHUSHA ALLIANCE

“Mpira ni mchezo wa makosa ukifanya kosa moja unaadhibiwa. Nakumbuka nikiwa Alliance nilifanya kosa ambalo sitalisahau, tulikuwa tunacheza Ligi Kuu Bara na Stand United. Ulikuwa ni mchezo wa kuamua nani ashuke,” anasema.

“Nakumbuka nilirudisha pasi fupi ambayo ilinaswa na mpinzani na kufunga bao nashukuru Mungu mchezo uliisha kwa sisi kushinda 3-2 lakini kwenye maisha yangu ya soka hilo ndio lilikuwa kosa langu la kizembe uwanjani.”

KAMBI POPOTE

“Nilisajiliwa Yanga baada ya kucheza vizuri nafasi ya kiungo mshambuliaji lakini nilipotua ndani ya timu hiyo nimecheza nafasi zaidi ya nne na zote nimecheza kwa usahihi.

“Nimecheza namba saba, nane, 10 na 11 na nimezitendea haki nafurahi nafasi hizo naweza kuzitumikia hadi nje ya Yanga ambayo walikuwa wananiamini na kunichezesha nafasi hizo. Mimi mpira ni kipaji sio wa kufundishwa japo ni muhimu na ndio maana kunakuwa na makocha kwaajili ya kutuongezea ujuzi.

“Pamoja na kupitia wakati mgumu kutokana na kutumikia msimu mmoja kati ya mitatu niliyosajiliwa Yanga. Napenda kuweka wazi kuwa nilifurahia maisha ndani ya timu hiyo kutokana na namna nilivyoishi vizuri na wenzangu.

Kipenseli anasema ni asilimia kubwa ya wachezaji hawakumuacha lakini amewataja Adeyum Salum na Abdulaziz Makame kuwa ni kati ya wachezaji ambao walikuwa karibu zaidi.

SOKA LIMEMPA KIWANJA

“Soka bado nalidai japo sio vibaya kusema nilichokivuna kwenye usajili wangu wa kwanza nilipata kiwanja cha Sh5 milioni ambachg najivunia. Nilichagua mpira ili kuendesha maisha yangu bila ya kumtegemea ndugu.

“Kwenye familia wazazi na ndugu wana umuhimu wa kusisitiza kitu kwa upande wangu walitamani sana nisome lakini akili yangu iliwekezwa kwenye soka na kujikuta nikishindwa kufanya vizuri masomo. Nilipewa kauli ngumu sana siwezi kuzisema lakini jibu langu lilikuwa ni moja naamini kwenye kile ninachokifanya.” anasema.

Chanzo: Mwanaspoti