Baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Singida Big Stars, Kelvin Nashoni ameibuka na kutaja sababu ya kutosaini Simba.
Nashoni ni kati ya wachezaji waliokuwa katika mazungumzo ya kujiunga na Simba katika usajili wa dirisha hili dogo kwa ajili ya kuimarisha safu hiyo ya kiungo mkabaji.
Kiungo huyo usajili wake ulipendekezwa na kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mgunda kwa ajili ya kusaidiana na Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Nashoni alikiri kufuatwa na mabosi wa Simba kwa ajili ya mazungumzo kwa ajili ya kumuhitaji katika kikosi chao.
Nashoni alisema kuwa ukweli ni kwamba walishindwa kufikia muafaka mzuri na Simba kusaini timu hiyo, katika dirisha dogo na kwenda kusaini Singida Big Stars.
Aliongeza kuwa maslahi mazuri ndio yamemfanya ashindwe kusaini mkataba Simba na kutua Singida Big Stars ambayo imempa dau na mshahara mnono.
“Tetesi zilikuwa nyingi za kunihusu mimi kwenda kusaini Simba, ambazo hizo ni kweli kabisa walinifuata na kushindwa kufikia muafaka mzuri.
“Nilitamani kusaini huko lakini ilishindikana, kwani Simba walishindwa kunipa maslahi mazuri na kuamua kuchukua maamuzi ya kusaini Singida Big Stars.
“Nimekuja hapa kupambania namba katika kikosi cha kwanza, nafahamu ushindani mkubwa lakini nitapambana,”alisema Nashoni.