Kiungo nyota wa zamani wa kimataifa wa Simba aliyewahi kutamba pia na timu za CDA na Taifa Stars, Mtemi Ramadhan ameipa nafasi kubwa Yanga kufanya vizuri katika mchezo wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi dhidi ya US Monastir ya Tunisia.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa leo kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Rades, uliopo mjini Tunis, Tunisia ikiwa ni mechi ya kwanza ya Kundi D lenye pia timu za TP Mazembe ya DR Congo na Real Bamako ya Mali.
Akizungumza Mtemi alisema sababu ya kuipa nafasi Yanga kufanya vizuri ni kutokana na wachezaji wake kujiamini na kucheza kitimu.
"Lazima tukubali Yanga sasa hivi wapo vizuri, timu yao inacheza na wamejua mashindano ya Kimataifa wanatakiwa kuchezaje," alisema kiungo huyo ambaye hata hivyo, ameitaka timu hiyo kuwa makini na Waarabu kwani wanajua kucheza mechi za nyumbani.
"Waarabu wanamtindo wao wa kucheza lazima wawe makini, wakija Dar es Salaam wawaige Simba pale hatoki mtu na wao wajitahidi asitoke mtu," alisema Mtemi aliyekuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki kwa mara ya kwanza Fainali za Afrika (Afcon) 1980 zilizofanyika nchini Nigeria.