Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiungo Simba: Soka la Bongo ni la Simba na Yanga tu

Morice Chukwuu Morice Chukwu

Fri, 12 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya Singida Fountain Gate kuyaaga mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea kule Zanzibar baada ya kufungwa kwa penalti 3-2, kiungo wa kikosi hicho cha wauza alizeti, Morice Chukwu amecharukia alichoita uonevu mkubwa waliofanyiwa akiwatuhumu waamuzi kuwabeba Wekundu wa Msimbazi.

Akizungumza na Mwanaspoti alisema mchezo ulikuwa mzuri na ingawa mambo ya uonevu hayawezi kukosekana katika mpira wa miguu ila kwa jana ilivuka mipaka.

"Hakuna kitu kingine wala timu nyingine zinazotakiwa kupata ushindi zaidi ya Simba na Yanga tu kwa nilivyoona, sina furaha na namna mambo yanavyokwenda, kwa njia hii timu hazitakuwa na mashindano kwani hakuna uhalisia wa mashindano," alisema Morice aliyejiunga na Singida msimu huu akitokea Rivers United ya Nigeria.

Alhamisi usiku, hadi kufikia dakika ya 90 ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, Singida ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 la straika Elvis Rupia aliyeitanguliza timu yake mapema akitumia vyema makosa ya beki wa Simba, Kennedy Juma, aliyetoa boko kwa kumpasia mpira mpinzani Marouf Tchakei jirani na boksi la Wekundu wa Msimbazi na kiungo huyo raia wa Togo kumpasia mpira mfungaji.

Ubao wa dakika za majeruhi ulionyesha dakika 8 zimeongezwa lakini ghafla zikabadilishwa na kuandikwa sita. Mwamuzi akaamuru mechi iendelee kuchezwa huku mara kwa mara wachezaji wa Singida wakimzonga kutaka amalize pambano. Hakulimaliza hadi Saido Ntibazonkiza alipopiga mpira akiwa amebanwa na mchezaji wa Singida. Mpira huo ulienda nje kabla ya kipa kuudaka akiwa nje ya uwanja na mwamuzi kuamuru kuwa ni kona. Wachezaji wa Singida walimzonga tena mwamuzi wakiamini mpira huo ulipaswa kuwa ni goal-kick, lakini mwamuzi alisisitiza ni kona iliyochongwa kiufundi na Saido Ntibazonkiza, ikaokolewa kwa kichwa na kutua mguuni kwa Fabrice Ngoma aliyeuweka wavuni. Wachezaji wa Singida wakamzonga kwa ghadhabu zaidi mwamuzi Nasri Siya 'Msomali' wakiongozwa na Hamad Wazir 'Kuku', ambaye angeweza hata kulimwa kadi nyekundu kwa vitendo vyake, lakini hakuonywa.

Mechi ikaamuliwa kwa penalti 3-2, huku straika wa zamani wa Simba, Meddie Kagere, akiwazamisha walima alizeti wenzake kwa kupiga penalti ya mwisho iliyokuwa kichekesho akimpasia mikononi kipa Ali Salim kwa shuti dhaifu.  

Ali Salim aliamua mechi hiyo kwa kudaka penalti tatu, lakini tuzo ya mchezaji bora ilienda kwa Kevin Kijili wa Singida ambaye aliondoka na zawadi ya Sh1 milioni.

Katika mahojiano ya mapema na Mwanaspoti, Hamad Wazir ambaye ni mume wa muigizaji Esha Buheti, alidai kwamba mechi hiyo ni bora isingefanyika. "Kama walipanga Simba ndio iende fainali ni bora wangetuambia mapema tusije uwanjani," alisema kwa hasira Kuku baada ya mechi hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live