Klabu ya Simba SC na Young Africans zinatajwa kupigana vikumbo kuiwania saini ya Kiungo wa Mabingwa wa Soka nchini Nigeria Morice Chukwu, ili acheze katika Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Michuano ya Kimataifa msimu ujao 2023/24.
Klabu hizo kongwe zinatajwa, kufuatia Kiungo huyo aliyekuwa kwenye kikosi cha Rivers United kilichoikabili Young Africans kukiri kuna uwezekano mkubwa mwezi Julai mwaka huu akawa kwenye uzi wa njano au mwekundu ndani ya ardhi ya Tanzania.
Kiungo huyo alitoa kauli hiyo baara ya mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Young Africans uliomalizika kwa sare ya 0-0, Jumapili (Aprili 30), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Hata hivyo Chukwu anadaiwa alianza kuzungumza na Kocha Mkuu wa Simba SC Robertinho na baadhi ya watu wanaosadikiwa kuwa wa klabu hiyo ya Msimbazi, lakini hawakufikia muafaka, lakini baada ya mchezo wa Jumapili Kocha Nabi nae akamuambia nia yake ya kutaka kumsajili.
Staa huyo ambaye anacheza kama kiungo mshambuliaji na mkabaji, amefichua mazungumzo yake na Kocha wa Simba, Robert Robertinho na jinsi Nasreeden Nabi wa Young Africans alivyomuita chemba baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.
“Nilizungumza na Kocha wa Simba SC kwanza kuhusiana na kujiunga na timu hiyo msimu ujao, lakini hata Young Africans baada ya mchezop wetu Kocha wao alinifuata tukazungumza, kwa jinsi ninavyoona nitakuja Dar es salaam Julai.”
“Ninaweza kusaini Simba au Young Africans, mpaka baadhi ya mashabiki wananiambia lazima uje, mimi sina tatizo, kuna uwezekano mkubwa nikasaini moja kati ya hizi timu mbili kwavile nimezungumza na makocha wao mambo mengi,” amesema Morice
Simba SC na Young Africans zimeanza kufanya usajili wa kimyakimya kujipanga kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Kimataifa. Watani hao wa jadi tayari wana uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kupitia ofa ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ambayo inaipa Tanzania nafasi nne za uwakilishi.