Simba washindwe wenyewe! Unaambiwa kiungo mkabaji tegemeo anayekipiga klabu ya Rivers United ya nchini Nigeria, Joseph Onoja amegoma kuongeza mkataba mwingine wa kuendelea kukipiga hapo.
Hiyo ni baada ya kupata taarifa za kuwepo katika mawindo na Simba katika usajili wa dirisha kubwa kwenye msimu ujao.
Simba imepanga kukifanyia maboresho makubwa kikosi chao katika usajili wa msimu huu na kati ya sehemu wanayoitazama ya kiungo mkabaji baada ya Ismael Sawadogo kushindwa kuonyesha ubora wake tangu ajiunge nao dirisha dogo.
Taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, uongozi wa Rivers United, ulimpa mkataba wa miaka miwili kiungo huyo kwa ajili ya kuusaini, lakini akagoma na kuomba kusubiria umalizike huo alionao ambao amebakisha miezi sita pekee.
Mtoa taarifa huyo, alisema kuwa ngumu kwake kwa sasa kuongeza mkataba mwingine huku akiwa ana ofa nyingi anazozipata na anazoendelea kuzipata ikiwemo kutoka Simba.
Aliongeza kuwa kwa sasa yupo tayari kufanya mazungumzo na klabu yoyote itakayohitaji huduma kwa ajili ya msimu ujao ikiwemo Simba iliyoonyesha nia.
“Onoja hivi sasa anachoangalia ni maslahi pekee na kikubwa anataka kuondoka kama akipata ofa nzuri kutoka kwa baadhi ya timu zitakazohitaji huduma yake.
“Juzi aligomea mkataba wa miaka miwili aliopewa na uongozi wake wa Rivers United, kwani hivi sasa amebakisha miezi sita ambao unampa ruhusa ya kuzungumza na klabu itakayomuhitaji.
“Amepata taarifa zayeye kuhitajika na Simba, kama yeye yupo tayari kujiunga nayo kama kweli inahitaji saini yake ili aondoke hapo Rivers United,” alisema mtoa taarifa huyo.
Championi Jumatano, lilifanya mazungumzo na meneja wa mchezaji huyo Ibrahim Sikiru na kusema kuwa: “Ni kweli Rivers United ilimpa mkataba mwingine wa miaka miwili kwa ajili ya kuendelea kubakia hapo.
“Lakini yeye amewaomba viongozi wasubirie hadi mkataba wake wa miezi sita utakapomalizika, kwani ana ofa nyingi ambazo amezipata na kama mazungumzo yakienda vizuri, basi huenda akajiunga na Simba,” alisema Ibrahim.