Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiungo Horoya aihofia Simba, yapewa mbinu

Simba Dubai Matata 1140x640 Kiungo Horoya aihofia Simba, yapewa mbinu

Thu, 9 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba inatupa karata yake ya kwanza kwenye hatua ya makundi, wakati itakapokabiliana na Horoya ya Guinea, kwenye Uwanja wa General Lansana Conte, uliopo mji mkuu, Conakry.

Wakati miamba hiyo ikikutana Jumamosi, kiungo nyota wa Horoya, Seyei Sebe Baffour ameelezea ugumu wa mchezo huo, huku akiweka wazi kuwa wanatarajia kupata ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wao ingawa malengo yao ni kutumia vyema uwanja wao.

“Simba ni timu kubwa ambayo imekuwa na rekodi nzuri inapocheza mashindano haya ya Afrika, hivyo tunawaheshimu sana, japo mchezo huu wa kwanza kwetu tunautumia kama njia mojawapo ya kutengeneza mazingira mazuri ya kundi letu,” alisema Seyei.

Baffour aliongeza kuwa wapo nyota wengi wa Simba wanao waangalia kwa umakini mkubwa kutokana na viwango vyao ingawa wao kama wachezaji wamejipanga kukabiliana na timu nzima kwa ujumla na wala sio kuangalia tu kiwango cha mchezaji mmoja mmoja.

Kwa upande wa nyota wa zamani wa Azam FC, Enock Atta Agyei ambaye msimu uliopita aliichezea Horoya alisema wachezaji wa Simba wanapaswa kujipanga vyema kwenye eneo la kiungo kwani wapinzani wao wana wachezaji bora wanaocheza maeneo hayo.

Katika michezo mitano iliyopita ya Horoya kwenye Ligi Kuu ya Guinea imeshinda miwili, sare mmoja na kupoteza miwili wakati eneo la ushambuliaji limefunga mabao matano na kuruhusu matatu, huku Simba katika mechi zake tano za Ligi Kuu Tanzania Bara imeshinda zote.

Simba inaonekana bora zaidi kwenye kuzifumania nyavu tofauti na wapinzani wao, kwani katika michezo hiyo mitano imefunga mabao 17 na kuruhusu matano.

Kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Simba iko kundi C na timu za Guinea (Horoya), Raja Casablanca (Morocco) na Vipers ya Uganda.

Simba imeondoka jijini leo mapema kuifuata miamba hiyo ya Guinea kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza wa Kundi C, ambao utachezwa Jumamosi.

Kocha wa Simba, Robertinho alisema juzi kuwa kikosi chake kitajitahidi kupata ushindi ugenini kama mipango yao walivyoiweka ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza robo fainali msimu huu.

YAACHA WATANO

Katika msafara wa nyota walioondoka leo, Simba imeacha wachezaji watano, akiwamo mkali wa mabao na asisti, Saido Ntibazonkiza, kwa kuwa majeruhi.

Wengine walioachwa ni Peter Banda, Israel Mwenda, Augustine Okrah na Jimmyson Mwinuke.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live