Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitunini: Nitafunga mabao 50 msimu huu

Kitunini.jpeg Fatuma Mustapha 'Kitunini'

Thu, 12 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mabeki wengi kwenye Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) wanamuelewa sana Fatuma Mustapha 'Kitunini' kutokana na uhodari wake wa kuzifumania nyavu.

Kwa msimu miwili amekuwa nje ya uwanja akiuguza majeraha ya goti aliyopata katika mechi ya sita tu ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo msimu wa 2020/2021 na hivyo kukaa nje msimu mzima.

Sasa msimu huu amerejea na katika mechi ya kwanza tu dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba Queens iliyofanyika Desemba 6 mwaka huu ametupia bao moja na kuiongoza timu yake ya JKT Queens kushinda mabao 2-1.

Fatuma anasema ndiyo amerudi hivyo, mabeki wa timu pinzani wajipange kwani anakitaka hasa kiatu cha dhahabu msimu huu.

Mchezaji huyo anasema amepanga msimu huu kufunga mabao 50, nusu kwenye mzunguko wa kwanza na nusu nyingine katika mzunguko wa pili na ikishindikana kabisa basi aweke nyavuni mabao 35.

MAJERAHA YALIVURUGA MIPANGO

"Msimu wa 2020/2021 nilipanga kufunga mabao 35 lakini nikaishia kufunga mabao 20 katika mechi tano tu za mwanzo wa ligi nilizocheza kwa msimu huo baada ya kuumia goti. "Ukweli nilijisikia vibaya kwani malengo yangu yalivurugika kwani nilikuwa na uhakika kabisa kuwa ningekuwa mfungaji bora."

Anasema anaushukuru uongozi wa timu yake ya JKT kwa kumhudumia muda wote alipokuwa anauguza goti lake kwani walimgharamia matibabu yote na kuhakikisha anarejea tena uwanjani. "Nilikaa nje karibu mwaka mzima na nusu na baada ya kupona mwaka jana Novemba nikaenda kozi ya kijeshi na nashukuru mazoezi ya kule yalinisaidia sana kuniweka fiti na ndiyo maana nimerejea uwanjani msimu huu," anasema Fatuma.

ANGUKO LA JKT

JKT Queens ilikuwa moja ya timu tishio sana miaka ya nyuma hasa kuanzia mwaka 2016 na walitwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu miwili mfululizo 2018/2019 na 2019/2020.

Hata hiyo, misimu mitatu iliyofuata timu hiyo ilionekana kama kushuka ubora wake na mara nyingi kuishia nafasi ya tatu jambo ambalo wadau wa soka la wanawake wamekuwa wakijiuliza je timu hiyo imepatwa na nini?.

"Hatujashuka kiwango lakini wengi wanaona hivyo kwa sababu ya kufananisha kile kikosi cha kipindi kile tunatwaa ubingwa mfululizo na kikosi cha misimu miwili iliyopita ambayo Simba imechukua ubingwa mfululizo ni tofauti kabisa.

"Ukiangalia ile timu yetu ya zamani, wachezaji wengi walitawanyika na kujiunga na timu nyingine tukabaki wachache na pia majeruhi walikuwa wengi kwani tulikuwa kama tunapokezana akiumia huyu mwingine anarudi uwanjani sasa hilo lilichangia kutuyumbisha.

"Hata hivyo, hatukufanya vibaya sana kwani kuna wakati tulimaliza wa pili na wakati mwingine wa tatu lakini sasa tunarejea kwa nguvu tukiutaka ubingwa msimu huu, "anasema Fatuma.

Anazungumzia pia juu ya msimu huu; "Zamani timu moja moja sana ndiyo ilikuwa na mchezaji wa kigeni lakini sasa hivi timu nyingi zina wachezaji kutoka nje ya nchi, sasa hali hiyo inafanya ligi kuwa na msisimko mkubwa na ushindani.

"Zama za timu kupigwa mabao mengi hazitakuwepo sana msimu huu labda unaweza ukaifunga timu pinzani bao tano ila ile ya kumpiga mtu 10 au 15 mh! safari hii naona itakuwa ngumu kwani timu nyingi zimefanya usajili wa maana ndio maana unaona ligi mwanzo tu imeonyesha ushindani mkubwa."

KUTUPIA MABAO HABAHATISHI

Anasema suala la yeye kuwa bora kwenye kufunga mabao halijaja hivi hivi bali ni kutokana na mazoezi makali anayofanya hasa na timu za wanaume. "Ukiondoa mazoezi ya timu pamoja na kufuata maelekezo ya kocha, huwa pia nafanya sana mazoezi binafsi.

"Kuna timu za kiume ambazo huwa nafanya nazo mazoezi zinanisaidia sana kuniweka fiti.Timu ya jeshi ya Green Warriors ambayo iko karibu na ninapoishi pia wakati mwingine tunacheza mechi na timu ya wanaume ya JKT Tanzania na timu nyingine ambazo huwa tunacheza nazo mechi ya kirafiki zinanisaidia kunipa mazoezi mazuri, "anasema Fatuma ambaye anamkubali beki wa kulia kutoka JKT Queens, Swaum Salum.

WACHEZAJI KWENDA NJE

Anafurahia jinsi wachezaji wa Tanzania wanavyokwenda kwa wingi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwani wataipa ubora timu ya Taifa.

"Kitu kizuri sana kwani uwepo wao uko utaiwezesha hata timu yetu ya Taifa kuwa bora kwa sababu kule wanapata vitu vingi vya kujifunza.

"Tanzania ina wachezaji wazuri sana na naamini kadri ligi yetu inavyoendelea kuwa bora basi wachezaji wengi watasajiliwa na timu za nje kama ilivyo hapa kwetu timu nyingi zimesajili wa kigeni, "anasema na kuongeza;

"Ingawa wachezaji hao wa kigeni waliosajiliwa na timu nyingi hapa nchini wengi wa kawaida tu kama sisi hawatuzidi sana wazawa lakini kwa sababu wamesajiliwa na kulipwa pesa nyingi inabidi wapangwe tu kikosi cha kwanza wacheze, "anasema Fatuma ambaye alipoulizwa kuhusu suala la yeye kucheza nje alikiri ni jambo gumu kutokana na aina ya kazi yake.

ATOA NENO

"Kama kutakuwa na wadhamini wengi, basi hata wachezaji watakuwa wengi kwa sababu ukienda kwenye ligi za mitaani huko kuna vipaji vikubwa sana kwa wanawake lakini wengi wanaogopa kucheza ligi kubwa kwa sababu wanaona hakuna watakachonufaika nacho.

"Angalau miaka miwili mitatu ya karibuni kuna mabadiliko. TFF wanajitahidi sana kuliinua soka la wanawake na niwaombe wasichoke, muhimu ni wadau wengine kuwaunga mkono kwa kujitokeza kusapoti ili ligi izidi kuwa bora zaidi, "anasema.

HUMWAMBII KITU KWA MAYELE

Kama kuna mchezaji ambaye Fatuma anamhusudu sana kwenye Ligi Kuu Bara ya wanaume sio mwingine bali ni Fiston Mayele wa Yanga.

"Yaani namkubali sana Mayele, analijua sana goli yule jamaa yaani nikimuona huwa ni kama najiona mimi uwanjani.

"Anajua kukaa katika nafasi, anajua apige wapi yaani akiwa ndani ya 18 ni ngumu kukosa, yaani yuko kama mimi na kuna vitu vingi naiga kutoka kwake. "Pia hata yule Moses Phiri naye ni mshambuliaji mzuri, ana kasi na uamuzi wa haraka akiwa ndani ya 18.

MPIRA UMEMPA AJIRA

Licha ya wazazi wengi kutaka watoto wao wasome na kuachana na mambo ya mpira lakini Fatuma anasema soka limempa ajira na anashukuru.

"Mpira wa miguu umenipa kazi hivyo watu wacheze hawawezi kujua ya mbele. Wazazi wasiwazuie watoto wao kucheza mpira, wawasapoti kuanzia kwenye masomo yao lakini wasisite kuwaunga mkono kwenye vipaji vyao. Mimi nilianza kucheza soka nikiwa shule ya msingi hadi sekondari na nilipenda tu kucheza.

"Nilishacheza klabu nyingi ikiwemo Sayari na kisha nikajiunga na Simba Queens na kuiwezesha kupanda Ligi Kuu lakini baada ya kuipandisha nikarudi Sayari baada ya hapo nikajiunga na Mburahati Queens ingawa hata ligi sikucheza kwani iliahirishwa na bahati nzuri kipindi hicho jeshini walitangaza nafasi za kazi na walikuwa wameanzisha timu yao ya wanawake wakatutafuta na wenzangu na kujiunga nao na ndio nipo hadi sasa."

KIKOSI CHAKE BORA

Najat Abbas (JKT Queens), Swaum Salum (JKT Queens), Wincate Kaari (Yanga Princess) Annastazia Katunzi (JKT Queens), Happness (JKT Queens), Amina Ally (Yanga Princess) Mwanahamis Omary ' Gaucho', Donisia Minja (JKT Queens), Fatuma Mustapha (JKT Queens), Opah Clement (Simba Queens) na Stumai Abdallah wa JKT Queens.

Chanzo: Mwanaspoti