Waziri Mkuu wa Hispania Pedro Sanchez ameingilia kati sakata la Rais wa Shirikisho la soka la nchi hiyo Luis Rubiales kumpiga busu mchezaji Jenni Hermoso, baada ya ushindi wa timu ya Taifa ya Hispania katika Kombe la Dunia la Wanawake lililomalizika huko Sydney, Australia.
Kwa upande wake, Bi.Hermoso ambaye ni nahodha wa timu na mfungaji maarufu wa magoli alinukuliwa akisema kuwa hakufurahia kitendo hicho. Waziri wa usawa wa Hispania, jana alikemea vikali kitendo hicho na kusema kuwa hakikubaliki.
Hapo jana, Rubiales alikiri kukosea na aliomba msamaha na kusema kuwa hakuwa na nia mbaya bali ilikuwa ni hisia za kusheherekea ushindi.
Hata hivyo Waziri Mkuu wa nchi hiyo amesema kilichotokea hakikubaliki na msamaha aliouomba Rubiales hautoshi, ” Ni lazima achukue hatua stahiki kuweka sawa kile tulichokiona”.
”Wachezaji wamefanya kila waliloweza mpaka kushinda, lakini tabia ya Rubiales inaonyesha kuwa bado tuna safari ndefu sana kuelekea kwenye usawa”.
Naye Naibu Waziri Mkuu wa Hispania Yolanda Diaz, amemtaka Rais wa Shirikisho hilo ajiuzulu.