Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitasa mwenye namba yake Singida

Carmo Kitasa mwenye namba yake Singida

Fri, 25 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kila nyumba ina kuta ambazo mwenye nayo anajisifia ni imara na ni sehemu ambayo inashirikiana na msingi kuhakikisha nyumba inakuwa imara.

Huku kwenye soka tukisema ukuta maana yake ni beki/mabeki wanaohakikisha timu yao hairuhusu mabao.

Kwenye kikosi cha Singida Fountain Gate zamani Singida Big Stars, kuna beki Biemes Carno anayefanya ukuta uwe imara mara zote.

Mwanaspoti linakuletea namna ambavyo Carno amekuwa mchezaji anayeunda ukuta bora tangu msimu uliopita akiwa anacheza sambamba na Pascal Wawa.

UHAKIKA WA NAMBA

Biemes kwenye eneo la ulinzi ndiye mchezaji pekee anayeanza kikosi cha kwanza cha sasa kati ya wale waliokuwa na uhakika msimu uliopita.

Benchi la ufundi limefumua safu ya ulinzi wa kikosi hicho na kucheza wageni wote isipokuwa Carno pekee.

Msimu uliopita eneo la mabeki walikuwa wanacheza Nicolas Gyan (kulia), Shafik Batambuze (kushoto), na mabeki wa kati ni Carno na Pascal Wawa.

Msimu huu wameingia wachezaji wapya, ambapo kulia anacheza Kelvin Kijiri, kushoto Gadiel Michael na beki wa kati akiingia Joash Onyango ila bado Carno ameendelea kupata nafasi.

Hii ni wazi kwamba amefanikiwa kulishawishi benchi la ufundi linaloongozwa na Hans Pluijm kumwamini.

KIONGOZI UWANJANI

Achana na kosa ambalo alifanya kwenye mechi ya Ngao ya Jamii walipocheza na Azam, Carno ataendelea kubaki kuwa kiongozi uwanjani.

Carno amekuwa mhimili wa kuituliza timu hasa inaposhambuliwa kwa kuanza kumtuliza kipa golini.

Beki huyu pia ni mwepesi wa kuanzisha mashambulizi pindi mpira unapokuwa langoni na lengo likiwa ni kuongoza timu.

Jambo hilo limemfanya aendelee kusalia kikosini kwa sababu amekua mzizi wa mafanikio tangu msimu uliopita.

MABAVU YENYE NGUVU

Sio kila beki wa kati anakuwa na mabavu na kutumia nguvu nyingi uwanjani, Carno amekudu kutumia nguvu na akili.

Carno ni beki mwenye mabavu anapokuwa uwanjani na hilo linamsaidia kwenye kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani.

Washambuliaji wa timu pinzani huwa na wakati mgumu wanapotana na beki huyo kutokana na namna ambavyo anavyokabiliana nao uwanjani.

Hata hivyo sio muda wote hutumia mabavu bali pale panapohitajika kutumika ndipo hufanya hivyo.

ANASHAMBULIA PIA

Carno licha ya kuwa na uwezo wa kuanzisha mashambulizi bado ana uwezo wa kushambulia pindi inapohitajika.

Beki huyu ana uwezo wa kuufanya uwanja kuwa mdogo kwa kuipeleka timu katikati ili kuwafanya washambuliaji wapeleke mashambulizi langoni kwa wapinzani.

Wakati huo huo Carno ni mzuri kwenye kushambulia hasa upande wa mipira kwenye mipira ya kona mara nyingi huwa anaenda kucheza mipira hiyo.

Urefu wake ndio silaha kubwa na amekuwa akiwapa presha mabeki wa timu pinzani kwenye mipira ya kona.

YEYOTE FRESHI

Baada ya kuwa na uhakika wa namba, Carno amekuwa akipangwa na mabeki mbalimbali na bado amefiti kucheza nao.

Msimu uliopita alicheza na Wawa lakini alipokosekana mwenzake basi alicheza na Ahmad Waziri au Abdulmajid Mangalo na wote alienda nao vizuri.

Msimu huu baada ya Wawa kuondoka Singida Fountain Gate, Carno anacheza na Joash Onyango huku wakiwa wanaelewana vizuri.

Onyango anapokosekana anaweza kucheza na Mangalo au Waziri na bado Carno amekuwa kwenye kiwango bora kuhakikisha eneo lao la ulinzi linafanya vizuri.

Chanzo: Mwanaspoti