Beki wa kati wa Azam FC, Malickou Ndoye ameonyesha nia ya kuondoka ndani ya timu hiyo baada ya msimu huu kumalizika kutokana na kutokuwa na uhakika wa kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata kutoka ndani ya timu hiyo zilieleza nyota huyo aliyekuwa nje ya uwanja tangu Oktoba mwaka jana kutokana na majeraha ya nyonga hayupo tayari kubaki licha ya mkataba wake kusalia mwaka mmoja zaidi baada ya msimu huu kumalizika.
"Mchezaji mwenyewe hayupo tayari kuchezea hapa kwa msimu ujao hivyo tunaendelea kusubiri kitakachojiri kati yake na viongozi, jambo analoliona ni kwamba ameshapoteza nafasi na anahitaji kupata changamoto mpya," kilisema chanzo hicho.
Akizungumzia hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' alisema suala la mchezaji kuondoka au kubaki bado hawajaanza mazungumzo nayo kwa sasa isipokuwa wanachokifanya ni kuboresha baadhi ya maeneo kwa ajili ya msimu ujao.
"Ni mapema sana kuzungumzia hilo japo tunatambua zimebaki mechi chache kumaliza msimu, tutakaa na benchi letu la ufundi na kusikiliza mapendekezo yake na baada ya hapo ndipo tutakuwa na wigo mpana sasa wa kuyazungumzia hayo," alisema.
Hata hivyo Mwanaspoti linatambua Azam tayari imeanza mipango ya msimu ujao na ujio wa beki mpya wa kati, Yoro Mamadou Diaby aliyesajiliwa akitokea Akademi ya Yeleen Olympique ya Mali ni ishara tosha ya kuondoka kwa Ndoye kikosini humo.
Yoro atakayeichezea Azam msimu ujao alikuwa kwa mkopo Klabu ya Stade Malien de Bamako aliyoisaidia kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika huku akiwa sehemu pia ya kikosi cha Mali kilichoshiriki CHAN, 2022 Algeria.