Baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Azam juzi, Kocha Msaidizi wa Namungo, Denis Kitambi amesema amefurahishwa na aina ya uchezaji wa nyota wa kikosi hicho kwani waliyafuata maelekezo yake vizuri.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kitambi alisema kitendo cha kutopata ushindi kiliifanya morali ya wachezaji kushuka kwa kiasi kikubwa ingawa alikaa nao chini na kuwajenga kisaikolojia jambo analoshukuru waliweza kumuelewa na kulionyesha uwanjani.
“Sio kwa kiwango kikubwa ila kupata ushindi mbele ya Azam sio jambo dogo kutokana na ubora waliokuwa nao, huu kwetu ni mwanzo tu na tunahitaji mwendelezo wa hili kwani itasaidia kuendelea kurejesha ari ya upambanaji kwenye timu,” alisema.
Kitambi aliyeiongoza timu hiyo baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Cedric Kaze kujiuzulu nafasi yake aliweka wazi licha tu ya ushindi huo ila bado wana kazi kubwa ya kufanya katika michezo ijayo ili kurejesha furaha iliyopotea kwa mashabiki zao.
“Kila mmoja wetu ana malengo yake aliyojiwekea na hivyo pia kwetu, msimu huu umeanza na ushindani kwa sababu timu zote zimejipanga vizuri, kadiri ambavyo ligi inazidi kusonga ndivyo ugumu nao unaongezeka hivyo ni muhimu kujiandaa mapema.”
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Namungo msimu huu katika michezo saba iliyocheza ya Ligi Kuu Bara ambapo wakati ikiwa chini Kaze ilishindwa kutamba kwani katika mechi sita alizoziongoza timu hiyo ilipoteza michezo mitatu na kuambulia pia sare tatu.
Namungo imeendeleza ubabe mbele ya Azam kwani mechi ya mwisho kabla ya hiyo iliyopigwa pia kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi Mei 14, mwaka huu ilishinda mabao 2-1, yaliyofungwa na nyota wa kikosi hicho, Hassan Kabunda na Shiza Kichuya.