Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitambi aanika tatizo Geita Gold

Dennis Kitambi Geita Gold FC Kitambi aanika tatizo Geita Gold

Sun, 26 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hatma ya Geita Gold kubaki Ligi Kuu msimu huu iko shakani kwani inalazimika kuifunga Azam FC keshokutwa iwapo haitaki kushuka daraja moja kwa moja na badala yake iangukie play-off, huku Kocha Mkuu, Denis Kitambi akifichua mambo mawili yaliyowakwamisha.

Geita ipo nafasi ya 15 na pointi 25 baada ya mechi 29, ikisubiri kumalizana na Azam katika mechi ya mwisho ya msimu itakayopigwa Uwanja wa Nyankumbu, Geita na iwapo itapoteza itaungana na Mtibwa Sugar kwenda moja kwa moja Ligi ya Championship.

Kipigo cha jana cha mabao 2-1 ikiwa kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa mbele ya Singida Fountain Gate, kimezidi kuliweka hatarini jahazi la timu hiyo na kocha Kitambi amesema wamejipanga kupambana ili kuinusuru timu, lakini akiweka bayana yanayomkwamisha hadi kuingia kwenye janga hilo.

Akizungumzia matokeo mabovu wanayoendelea kuyapata, Kitambi, amesema usajili ambao haukukidhi matarajio na ubutu kwenye safu yake ya ushambuliaji ndiyo mambo makubwa ambayo yamekuwa kikwazo kwao msimu huu.

"Suala la usajili nadhani ni moja ya sababu, kingine ni kwamba hatujatumia nafasi zetu ambazo tumezitengeneza kwa sababu ukiangalia mechi tulizocheza nimezirudia zaidi ya mara tano kuziangalia kila mechi tunatengeneza nafasi," amesema Kitambi na kuongezea;

"Hata mchezo wa leo (jana) tumetengeza nyingi kuliko mpinzani lakini hatujafunga hicho ndicho kimekuwa kikwazo kikubwa kwetu. Mwalimu anakuwa na imani amefanya kazi ya kutosha ya kushinda mchezo lakini huwezi kuwa na uhakika kwa sababu kuna mtu wa tatu uwanjani pale."

Kuhusu mchezo wa Azam, Kitambi amesema "Tumejiweka katika nafasi ngumu sana, sasa ni lazima tushinde mchezo wa mwisho lakini tukiwa tunaomba wapinzani wetu angalau wapoteze tupate nafasi ya kucheza play-off."

"Timu inapofungwa kocha ndiye unabeba lawama zote lakini ikishinda ni wachezaji, lazima niwajibike kwa kiwango cha timu kwa hiyo tutaangalia nini tunaweza kurekebisha katika siku moja iliyobaki kwa ajili ya mchezo wetu wa mwisho," amesema Kitambi.

Kitambi aliyekabidhiwa Geita, Desemba 21, 2023 akichukua nafasi ya Hemed Suleiman 'Morocco', ameiongoza timu hiyo katika michezo 16 ya Ligi Kuu na kushinda mbili, sare sita na kupoteza nane, huku ikifunga mabao 10 na kuruhusu 22.

Chanzo: Mwanaspoti