Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitambi aachiwa msala Namungo

Denis Kitambi 1080x640 Kitambi aachiwa msala Namungo

Tue, 14 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Uongozi wa Namungo FC huenda ukamuamini Kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Denis Kitambi na kumkabidhi mazima timu baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa kocha mkuu Mrundi Cedric Kaze.

Kaze aliyewahi kuinoa Yanga alijiuzulu Namungo Oktoba 22, kutokana na muenendo mbaya wa timu hiyo na nafasi yake kukaimiwa na Kitambi aliyekuwa kocha msaidizi wa wauaji wa kusini.

Katika kipindi cha kukaimu nafasi hiyo, Kitambi ameingoza Namungo mechi tatu za Ligi Kuu mfululuzo ugenini, akishinda moja 3-1, dhidi ya Azam, na kutoa sare mbili, 0-0, mbele ya Coastal Union na 1-1, dhidi ya Simba matokeo yaliyowashawishi mabosi wa timu hiyo na sasa wanataka kupiga 'stop' zoezi la kutafuta kocha mpya.

Moja ya viongozi wa Namungo licha ya kutotaka jina lake litajwe, aliliambia Mwanaspoti muenendo wa Kitambi huenda umewafanya wampe muda zaidi.

"Hakuna timu inapenda kubadili kocha mara kwa mara, ni kweli baada ya kuondoka kwa Kaze tulipanga kuleta kocha mpya, lakini muenendo wa Kitambi umetufanya tuanze kuwaza kuachana na kocha mpya na kumpatia timu mazima, huenda ikawa hivyo kwani tutakaa vikao katika siku mbili hizi kuamua hili," alisema kiongozi huyo.

Namungo ipo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi na alama nane baada ya mechi tisa ikishinda moja, sare tano na kupoteza tatu, na mechi zijazo itakutana na Ihefu Novemba 23 kisha Geita Novemba 26 mwaka huu.

Ofisa Habari wa Namungo FC, Kindamba Namlia alisema; “Taarifa iliyotolewa mwanzo ni hiyo hiyo, Kitambi ataendelea kuongoza timu, kama yakitokea mabadiliko, tutawaambia.”

Chanzo: Mwanaspoti