Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitambaa cha unahodha Azam kimepata mwenyewe

Daniel Amoah Capt Daniel Amoah

Wed, 11 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Ligi Kuu ikisimama kupisha ratiba za timu za taifa, pale Azam FC mastaa wa kikosi hicho wanaenda mapumziko wakimjua nahodha mkuu mpya wa chama hilo linaloshika nafasi ya pili baada ya mechi tano za mwanzo wa ligi.

Tangu kuondoka kwa Agrey Morris aliyekuwa nahodha wa muda mrefu wa Azam, sambamba na msaidizi wake Mzimbabwe Bruce Kangwa, hatimaye Azam imepata nahodha mpya rasmi.

Baada ya wawili hao kuondoka kikosini hapo mwishoni mwa msimu uliopita, kitambaa cha unahodha kilivaliwa na Sospeter Bajana ambaye baadhi ya mashabiki wa Azam waliamini atakuwa mrithi wa Agrey kuwa nahodha mkuu lakini ghafla mambo yamebadilika.

Ukiachana na Bajana, wengine waliokuwa wakivaa kitambaa hicho tangu timu hiyo imekabidhiwa kwa kocha Msenegal Youssouph Dabo, ni Idriss Mbombo, Yahya Zayd na Daniel Amoah.

Moja ya wachezaji wa Azam (jina tunalo), alilithibitishia Mwanaspoti, nahodha mpya wa chama hilo kwa sasa ni Daniel Amoah licha ya kwamba awali ilipangwa awe Bajana.

“Mwanzo kocha alikuwa hana nahodha mpya, alimpa kitambaa mtu yeyote aliyejisikia, baadaye kikarudi kwa Bajana lakini kuna mambo yametokea amebadilisha na ametutangazia nahodha mkuu ni Amoah,” alisema mchezaji huyo na kuongeza;

"Pia wasaidizi watakuwa Mbombo, Bajana na Yahya.”

Azam FC msimu huu ina lengo la kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya pili baada ya kuutwaa mara ya kwanza msimu wa 2013/2014.

Chanzo: Mwanaspoti