Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitakachozibeba Simba na Yanga wiki hii

Simba, Yanga Warejea Ligi Kuu Wikiendi Hii Kitakachozibeba Simba na Yanga wiki hii

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Simba na Yanga zikijiandaa na mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwishoni mwa wiki hii, takwimu zinaonyesha timu hizo ziko vizuri na ni bora kimatokeo ikilinganishwa na Asec Mimosas ya Ivory Coast na CR Belouizdad ya Algeria kwa kuzingatia mienendo ya kila moja katika michezo mitano iliyopita ya mashindano tofauti.

Keshokutwa, Ijumaa kuanzia saa 4:00 usiku, Simba itacheza na Asec Mimosas na Jumamosi, Yanga itakuwa nyumbani kuikaribisha CR Belouizdad kuanzia saa 1:00 usiku.

Simba imekwenda Ivory Coast ikiwa imeimarika chini ya kocha Abdelhak Benchikha ambaye amerejesha morali ya timu, huku ikiwa na mwenendo mzuri katika michezo mitano iliyopita ambapo haijapoteza hata mmoja, ikishinda mara nne na kutoka sare moja.

Wacheaji wa Simba wamefunga mabao manane kwenye michezo mitano wakiwa na wastani wa bao 1.6 la kufunga kwa mchezo huku nyavu zao zikiguswa mara moja ikiwa ni wastani wa bao 0.2.

Asec Mimosas katika michezo yake mitano iliyopita ambapo imeshinda mechi mbili, imetoka sare moja na kupoteza mbili.

Timu hiyo ambayo inaongoza msimamo wa kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi 10, imefunga mabao matano katika michezo mitano iliyopita ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kwenye kila mchezo na imeruhusu mabao matatu ikiwa ni wastani wa bao 0.6 kwa kila mechi.

Kwa upande wa Yanga, takwimu zinaibeba kwani kwenye michezo mitano iliyopita kabla ya jana usiku dhidi ya Polisi Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), imepata ushindi mara nne na sare moja.

Yanga ina wastani wa kufunga kama wa Simba bao 1.6 kwa kila mchezo huku ikiwa na wastani wa kuruhusu bao 0.4 kwa mechi. Kwa upande CR Belouizdad, takwimu si haba kwenye upachikaji wa mabao kwani ina wastani wa kufunga bao 1.6.

Katika michezo mitano iliyopita kwenye mashindano yote, CR Belouizdad imeshinda mitatu, ikitoka sare mmoja na kupoteza mmoja.

Takwimu za mechi tano zilizopita zinaonyesha kuwa Asec Mimosas ni timu yenye uwezo wa kufunga zaidi katika kipindi cha kwanza kwani katika mabao matano iliyo nayo zaidi ya nusu (matatu) yamefungwa kipindi hicho huku mawili ikifunga cha pili.

Wakati Asec Mimosas ikionekana kuwa hatari katika kipindi cha pili pia inaonekana kuwa timu ambayo inafungika kipindi hicho kwani kati ya mabao matatu iliyoruhusu mawili yamefungwa kipindi cha kwanza huku moja likiwa la kile cha pili.

Kwa upande wa Simba inaonekana kuwa ni timu isiyotabirika, hivyo Asec Mimosas inaweza kuwa na wakati mgumu kuidhibiti kwani kati ya mabao manane iliyo nayo, manne imefunga kipindi cha kwanza na mengine cha pili.

CR Belouizdad ambayo ipo katika nafasi ya pili kwenye kundi D ikiwa na pointi tano sawa na Yanga, ni timu ambayo inaonekana kuwa hatari kipindi cha pili kwani katika mabao manane iliyofunga kwenye michezo mitano iliyopita, matano imefunga kipindi hicho.

Akizungumzia mchezo wao na Asec mimosas, kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola amesema wameenda kutafuta matokeo ya ushindi wakiamini kwamba ni mechi ngumu, lakini kama timu wapo tayari kwa ajili ya kukabiliana na ugumu huo, kwani kucheza ugenini sio tatizo maana mpira siku hizi hauna cha ugenini wala nyumbani.

Kwa upande wake, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema: “Kila kocha ana malengo mazuri kwenye timu anayopewa majukumu. Naamini ubora wa kikosi nilicho nacho tunaweza kufanya mambo makubwa na ya kushangaza kama ilivyokuwa hatua ya makundi.”

Chanzo: Mwanaspoti