Kipa Jonathan Nahimana amesema siri kubwa ambayo inamfanya aendelee kuwa katika kiwango kikubwa ni kufahamu akiteleza anapoteza nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza.
Nahimana ndiye kipa namba moja kwenye kikosi cha kwanza kwa misimu miwili mfululizo akiwa na timu hiyo.
Akizungumza Nahimana alisema anapambana sana na kufanya mazoezi kwa bidii kwa sababu anajua yupo David Kissu ambaye na yeye anafanya vizuri.
“Siri yangu napambana sana nafanya mazoezi kwa bidii kwasababu najua mtu ambaye nacheza naye nafasi moja sio mbaya ni kipa mzuri ndio maana ananipa changamoto nzuri” alisema Nahimana na kuongeza;
“David ana umbo na kimo ambacho kinamfanya awe kipa mzuri, kingine amecheza nje ya nchi kwahiyo na uzoefu mwingine wa ziada.”
Kissu licha ya kwenda Namungo kwa mkopo hajaweza kupenya katika kikosi cha kwanza mbele ya Nahimana ambaye hata msimu uliopita alimuweka benchi Nurdin Balora.
Nahimana ameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa Burundi kwa ajili ya michezo ya kirafiki ya kalenda ya FIFA.