Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisinda wa leo sio Moloko wala Lunyamila

Kisinda Pic 1 Kisinda wa leo sio Moloko wala Lunyamila

Mon, 21 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ni Februari 23, 2021 mpira unakwisha katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar e Salaam. Al Ahly ya Misri imekubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji wao, Simba Sports Club.

Mashabiki wa Mnyama wanashangilia kwa shangwe na vifijo kupita kiasi. Wengine wa upande wa pili wamenuna. Utadhani timu yao ndiyo imefungwa.

Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali wanakusanyana kumfuata Kocha wa Al Ahly, Pitso Masomane kwa shauku kubwa - swali moja tu mioyoni mwao linalomhusu mfungaji wa bao la Simba katika dakika ya 38, raia wa Msumbiji, Luis Miquissone.

Miquissone alifunga bao hilo katika wakati mgumu. Alizunguka katikati ya msitu wa wachezaji wa Al Ahly na kuachia shuti la mita 20 lililojaa kimiani.

KWANINI ALIMUACHA?

Waandishi wote wanataka kujua kwanini Pitso Mosimane aliamuacha na kuishia kumtoa kwa mkopo mchezaji huyu mfupi machachari akiwa kocha wa Mamelodi Sundowns pale Afrika Kusini.

Mosimane alimtoa mchezaji huyo kwa mkopo katika timu kadhaa za Afrika Kusini ikiwamo Chippa United, Royal Eagles na baadaye akamrudisha kwa timu ya nyumbani kwao, UD Songo na hatimaye akatua Simba mwaka 2020.

Kwa Watanzania, Miquissone ni bonge la mchezaji. Ni aina ya wachezaji ambao wengi wanawapenda na inadaiwa Simba iliwazidi ujanja wapinzani wao wa jadi, Yanga katika kuinasa saini yake.

MSIKIE MASOMANE SASA

Kocha Mosimane alijibu kiu ya waandishi wa habari. Aliwaambia hakuwa na muda na mchezaji huyo kwa kuwa alikuwa akikimbia tu na mpira.

Mosimane alisema mpira wa kisasa haupo hivyo. Wakati wewe unakimbia nao kuna mtu yuko kwenye nafasi ya kuupokea na kutengeneza shambulizi la uhakika. Alisema kukimbia na mpira hakuna maana kwa kuwa kunachelewesha mashambulizi ya uhakika zaidi.

ULIWAHI KUSIKIA HII

Miquissone sio aina ya wachezaji wanaofaa katika staili ya kuichezea Simba. Ni wachache wa aina yake waliwahi kuichezea timu hiyo. Kwa uchache nitawataja, Sunday Juma, Itutu Kiggi na Ibrahim Malekano.

Lakini wachezaji wa aina yake wengi waliichezea Yanga. Mabingwa hao wa kihistoria wanaamini wachezaji wa aina na Miquissone ndio wanaopaswa kuwa nao katika winga ya kushoto au kulia. Usibishe.

WENGINE HAWA HAPA

Staili ya Miquissone ni kama ile ya Jonas Lunyamila, Said Maulid, Mrisho Ngassa, Justine Mtekele, Celestine ‘Sikinde’ Mbunga na Omary Hussein ‘Keegan’.

Bado kuna huyu mwingine, Simon Msuva. Ulishawahi kuwasikia mashabiki wa Yanga wakilalamika baada ya Msuva kuuzwa nchini Morocco kwa timu ya Difaa El Jadida.

Wengi walikuwa wakilalamika kwa kukosekana winga wa kukimbiza kama mbadala wa Msuva.

Timu ilipompata Tuisila Kisinda kila mtu aliona ndiye aliyestahili hasa kucheza katika timu yao kwa sababu ana spidi, anakimbia kama Lunyamila, kama Msuva, kama Ngassa, kama Said Maulid na wengine wengi.

KISINDA V ONYANGO

Mashabiki wa Yanga walifurahi Kisinda alipokuwa akimkimbiza beki wa Simba, Mkenya Joash Onyango. Walikuwa wakikumbuka vita ya Lunyamila dhidi ya mabeki Kassongo Athuman na Twaha Hamidu ‘Noriega’ na hata Abubakar Kombo.

Kisinda alisababisha Onyango kuipa Yanga penalti, lakini Lunyamila alisababisha kadi nyekundu kwa Kasongo Athumani mara mbili. Wakati beki huyo alipo-kuwa akiitumikia Sigara na hata Simba.

Mwishoni mwa msimu wa 2021/ 22, Yanga ilimuuza Kisinda. Haikuchukua muda wakampata mbadala wake. Jesus Moloko.

Ulishawahi kukaa karibu na shabiki au mwanachama wa Yanga alivyokuwa akimsifia Moloko.

“Kaka kwa huyu Moloko? Kisinda cha mtoto. Huyu ni hatari zaidi. Onyango kazi iko palepale.”

KISINDA KABADILIKA?

Ratiba ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ilipotoka na Simba kupangwa na RS Berkane ya Morocco.

Klabu anayoichezea Kisinda, mashabiki wa Yanga wakasema Onyango kazi iko palepale siku ya mechi baina ya timu hizo. Walijua Kisinda a.k.a Turbo angemkimbiza tena Onyango.

Katika mchezo wa kwanza wa timu hizo kule Morocco, mashabiki wa Yanga waliopo nchini walijaa katika runinga zao kutaka kushuhudia Kisinda akimkimbiza Onyango, lakini mambo yalikuwa tofauti.

Kisinda mpya alikuwa amezaliwa. Hakuwa akikimbia na mpira kama ilivyotarajiwa na wengi. Hakumkimbiza Onyango wala Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

NYEMBELA ALIWAKILISHA MAWAZO YAO

Mwandishi wa Kampuni ya Utangazaji wa Azam, Patrick Nyembela aliyekuwa ameambatana na Simba nchini Morocco naye alikuwa na shauku kama ya wale mashabiki wengine.

Hakumfuata Kocha Florent Ibengé, moja kwa moja kwenye kipaza sauti alikuwa ni Kisinda mwenyewe. Unajua alimuuliza nini? Kwanini hukimbizi kama kule?

Kisinda alijibu kuwa ule sio mpira. Mpira wa kisasa unacheza kwa nafasi na kutafuta kuingia kwenye boksi.

YANGA BADO INAHITAJI LUNYAMILA?

Soka la zamani, makocha walikuwa wakiziandaa timu kwa ajili ya msimu mzima. Soka la kisasa makocha wanaziandaa timu kucheza kwa mbinu na ufundi dhidi ya timu wanazokutana nazo wiki hadi wiki.

Makocha wanaangalia udhaifu wa timu pinzani na makali yao yako wapi na kuwapa majukumu wachezaji wao.

Hata kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi naye ameanza kubadilika na kutafuta mbinu zaidi katika kusaka ushindi. Nabi si muumini wa soka la Moloko.

Ndio maana leo kuna wachezaji wengi wanaocheza na winga zaidi ya Moloko. Kuna Chico Ushindi, Denis Nkane, Farid Mussa na hata Dickson Ambundo.

Kumbuka, Kisinda alikuwa akitumika kama silaha ya maangamizi. Mpira unapigwa mrefu anakimbia peke yake kwenda kuleta madhara kwa mpinzani.

FUNZO KUBWA

Kwanza makocha wetu wabadilike. Wafundishe kwa mbinu, waachane na tabia ya kuwajaza wachezaji stamina na pumzi kisha kuwaacha wanatumia mbinu zao binafsi ‘individual skills.

Hata Lunyamila angekuwepo leo angebadilika. Ushahidi wa hilo uko kwa Msuva. Sio tena mchezaji wa kuchukua mpira na kukimbia nao kwenye kibendera ya timu pinzani.

Msuva kaenda Morocco na kukutana na timu zinazocheza kisasa zaidi na kumbadilisha, akitumika kama mshambuliaji wa kati na hata akicheza pembeni leo hakimbiikimbii ovyo, bali anacheza kwa nafasi kwa nia ya kuisaidia timu, huku akifunga mabao.

Ndivyo anavyotumika pia ndani ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’ anafunga na kuasisti bila kutumia kasi aliyokuwa akicheza nayo wakati akiwa Jangwani.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz