Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisa usajili, Simba vijana yagoma kucheza na Yanga Dar

Kisa Usajiliiii Kisa usajili, Simba vijana yagoma kucheza na Yanga Dar

Sun, 29 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mechi ya ligi ya vijana chini ya miaka 20 kati ya Yanga na Simba iliyokuwa ifanyike juzi, Ijumaa kwenye viwanja vya TFF Kigamboni, Dar haikufanyika.

Mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa saa nane mchana ilikwama baada ya Simba hadi ipate uthibitisho kwamba Yanga ilifanya usajili halali wa wachezaji wote.

Ni jambo la kushangaza kwamba Simba ilikataa kucheza. Hata kama ni kweli Yanga haikusajili, Simba inawahusu nini? Kwanini isikubali kucheza chini ya angalizo halafu ikitokea ikabainika kweli Yanga haikusajili, basi ipewe ushindi mezani endapo itapoteza uwanjani?

Hapo ndipo inapokuja hoja Simba na Yanga zinayumbisha mamlaka za soka nchini. Timu hizo zinaweza kuzua mgogoro usio na kichwa wala miguu na kuchafua hali ya hewa.

SIMBA

Simba ilikataa kucheza mechi hiyo kwa sababu binafsi kuliko ilizotaja. Ukweli ni kwamba ilikataa ikihofia kudhalilika kwa sababu haikujiandaa.

Timu ilikusanywa siku tatu kabla ya kuanza kwa msimu ambapo ilicheza na Namungo na kufungwa bao 1-0.

Baada ya kuiangalia timu ikaona kuna kila dalili ya kudhalilika kwenye mchezo huo ambao hauna timu za watoto wala wakubwa kutokana na historia ya utani.

Kwa hiyo ikatengeneza ‘haka kasababu’ ili ipate pa kujifichia. Licha ya udhamini mkubwa kwa timu ya vijana, Simba hana mradi wa maana kwa vijana zaidi ya ujanja ujanja na kuwekeza kwenye timu kubwa. Iliwatangaza kwa mbwembwe Selemani Matola na Patrick Rweyemamu kuwa kocha na meneja mtawalia, lakini hawajawezeshwa kufanya kazi inavyotakiwa.

Mchezo wa kwanza dhidi ya Namungo uliofanyika Oktoba 22 palepale TFF Kigamboni ulitoa picha halisi ya kukosa utayari kwa timu hiyo. Ilicheza kwa kiwango cha chini huku hata wachezaji wenyewe wakiwa hawajuani vizuri. Mara nyingi walikuwa wakiitana ‘oyaa’ badala ya majina kama timu zingine. Huko kutojuana vizuri kulijionyesha hata kwenye uchezaji, haikuonekana kama timu iliyokaa pamoja muda mrefu.

YANGA

Taarifa za ndani zinaeleza kwamba licha ya Simba kujificha kwenye kichaka cha usajili, lakini ni kweli kwamba Yanga haikusajili wachezaji wake. Japo taarifa za usajili zinafichwa na TFF, inasemekana haikuwa na timu ya vijana hadi dirisha la usajili linafungwa.

Mashindano yalipokuja wakakusanywa vijana na kuunda timu. Kuanzia hapo wakaanza harakati za kufanya usajili nje ya dirisha kwa kushirikiana na baadhi ya watu katika mamlaka.

Wakati harakati hizo zikiendelea ndipo Simba wakapata taarifa za ndani kutoka hukohuko wakifaidika na Usimba na Uyanga. Hii ni kawaida kwa taarifa za pande hizo kuvuja hasa mtendaji mmoja wa juu akiona kuna jambo ambalo timu yake inaweza kufaidika.

Agosti 2014, mtendaji mmoja wa juu kwenye soka, alivujisha taarifa ya usajili wa Emmanuel Okwi aliyekuwa Yanga. Okwi ambaye awali alikuwa Simba kabla ya kwenda kujaribu bahati Austria ambako alifeli na nafasi yake kuchukuliwa na Sadio Mane, akarudi Uganda kisha akajiunga na Yanga, Januari 2014.

Lakini baada ya msimu Yanga wakataka kumuacha kwenye usajili bila kumpa taarifa ili asiende Simba. Yule mtendaji ambaye ofisi yake ilihusika na mambo ya sheria, aliwatonya Simba. Simba hawakushangaa wakamchukua. Sasa uvujaji wa taarifa wa aina hii ndiyo uliofanyika kwenye sakata hili la usajili wa wachezaji wa timu za vijana.

Baada ya Simba kupata taarifa Yanga haijafanya usajili wa wachezaji, ikasimamia hapo hapo kukwepa aibu.

MAMLAKA

Mamlaka za soka nchini zimekosa namna ya kujinasua kutoka janga hili kwa sababu zimemezwa na klabu hizi.

Watendaji wa mamlaka wanatoka klabu hizi mbili na wanashindana kwa ushabiki. Ni fahari kwa mtendaji wa mamlaka kujinasibu rangi anazoshabikia bila kuhofia nafasi yake. Kwenye vikao vyao wanatumia muda mwingi kutaniana kwa rangi zao kama unavyoona bungeni wabunge wanavyotaniana.

Hata kwenye hili sakata la Simba kugomea mchezo mamlaka haijui ifanye nini au ianzie wapi. Hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na wala hakuna hatua zilizochukuliwa hadi wakati wa kuandika makala hii. Mamlaka zinaogopa kufanya chochote zisije zikachafua hali ya hewa kipindi hiki cha utulivu.

Ni kweli kwamba Yanga haijasajili wachezaji, lakini unawafanyaje kuiondoa kwenye ligi? Si utaharibu uhusiano mzuri uliopo sasa ambao mamlaka zinaufurahia? Simba haikupaswa kugomea mechi kwa sababu ya usajili kwa kwa kuwa siyo jukumu lao. Lakini unafanyaje ilhali ni kweli Yanga hawakusajili.

Ukiwaadhibu Simba halafu ikabainika Yanga haikusajili na mlitaka kufanya njama ya kuhalalisha haramu si itakuwa balaa pia? Matokeo yake sasa mamlaka ziko njia panda.zinayumbishwa na timu hizo mbili.

UNAIKUMBUKA HII?

Mwaka 2008, Simba na Yanga zilitakiwa kukutana kwenye mechi ya kutafuta mshindi wa tatu wa Kombe la Kagame mashindano yaliyofanyika Dar es Salaam. Awali zilitakiwa kukutana kwenye nusu fainali kutokana na matokeo ya hatua ya robo fainali, lakini kwa ushawishi wa TFF, Cecafa ikabadilisha ratiba.

Mshindi wa robo fainali ya kwanza (Simba 2-0 APR) alitakuwa kukutana na mshindi wa robo fainali ya tatu (Yanga 2-0 Vital’O). Halafu mshindi wa robo fainali ya pili (URA 2-0 Miembeni) alitakiwa kukutana na mshindi wa robo fainali ya nne (Tusker 0-0 Rayon Sport [7-6 pen]).

Kwa hiyo Simba baada ya kushinda robo fainali ya kwanza dhidi ya APR ikatakiwa kukutana na Yanga ambayo ilishinda robo fainali ya tatu dhidi ya Vital’O. Lakini mamlaka wakatengeneza ushawishi. Ushawishi kwa Cecafa ulijengwa kwa hoja ya kwamba Yanga na Simba zikikutana fainali kutakuwa na mvuto mkubwa.

Wakasahau kwamba mpira ni sawa na maji ya mafuriko, hayapangiwi njia ya kupita, kwani yanapita yanakotaka.

Simba ikabadilishiwa mpinzani ikapangwa na URA ya Uganda ikafungwa bao 1-0 na kutolewa. Yanga nayo ikacheza na Tusker ikafungwa 1-0 na kutolewa.

Ndipo zikajikuta zinatakiwa kukutana kutafuta mshindi wa tatu. Mechi iliyotakiwa kuwa ya nusu fainali lakini ikatamaniwa iwe fainali, ikaangukia kuwa ya kutafuta mshindi wa tatu.

Lakini Yanga iliathirika sana na nusu fainali dhidi ya Tusker. Wachezaji wake wengi waliumia hivyo kikosi hakikuwa na nyota wanaotegemewa.

Kucheza na Simba kwenye mazingira kama hayo ni kujitafutia aibu ya bure. Yanga wakautumia vizuri ule msemo wa Kiswahili wa bora lawama kuliko fedheha wakakataa kucheza mechi hiyo.

Miaka zaidi 15 baadaye, Simba wanasawazisha kwa kukataa mechi dhidi ya Yanga, lakini safari hii kwa timu ya vijana.

Chanzo: Mwanaspoti