Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisa kamari... Paqueta hatarini kufungiwa miaka 10

Lucas Paqueta Matatani Kisa kamari... Paqueta hatarini kufungiwa miaka 10

Sat, 25 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Lucas Paqueta, anaweza kuwa kwenye hatua ya mwisho kabisa ya soka lake endapo atakutwa na hatia ya kucheza kamari huku akiwa anaitumikia West Ham kwenye michezo kadhaa ya Ligi Kuu England.

Shirikisho la Soka la England FA limeanzisha uchunguzi kuhusu kadi nne za njano ambazo amepewa mchezaji huyo kuanzia mwaka 2022-2023, kama alipewa makusudi kwa kuwa alikuwa amecheza kamari na akikutwa na hatia atafungiwa miaka 10 kujihusisha na soka.

Paqueta ambaye anatajwa kuwa mchezaji mahiri zaidi wa West Hama tangu aondoke Dimitri Payet, lakini pamoja na umahiri wake amekuwa akitia shaka kutokana na aina ya kadi ambazo amekuwa akipewa uwanjani.

FA imeanza uchunguzi kuhusu kadi alizopewa kwenye mchezo dhidi ya Leicester, Aston Villa, Leeds na Bournemouth ikidaiwa kuwa kuna uwezekano alifanya makosa makusudi ili apate fedha kwenye kamari au rafiki zake.

Inaelezwa kuwa FA wamefanya uchunguzi wao kwa miezi tisa kuanzia Novemba 2022 hadi Agosti 2023 na sasa wameanza mashtaka juu ya staa huyo ambaye alihusika kuipa West Ham ubingwa wa Europe Conference msimu uliopita.

Taarifa ya FA, inasema kuwa uchunguzi umeonyesha kuwa aidha ni mchezaji huyo au rafiki zake wamefaidika na kadi hizo ambazo waliziwekea fedha kwenye makampuni ya kubashiri michezo.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa mchezaji huyo amehojiwa na amekanusha tuhuma zote huku klabu yake ya West Ham ikimuunga mkono kwa asilimia 100.

Kama staa huyo atakutwa na hatia anaweza kukumbana na adhabu kubwa kama ambavyo alifungiwa beki wa Reading Kynan Isaac miaka kumi baada ya kupewa kadi kwenye mchezo kati ya timu yake ya Stratford Town dhidi ya Shrewsbury kwenye mchezo wa FA miaka mitatu iliyopita na kubainika kuwa aliibashiria kadi hiyo.

"Nimeshangazwa sana kuona FA imeamua kunishtaki, kwa kipindi cha miezi tisa nimekuwa nikiwapa ushirikiano mkubwa sana kwenye kila hatua ambayo nimekuwa nikiwapa kila taarifa ambayo wanaitaka.

"Nimeyakataa mashtaka yote na nitapambana kwa nguvu kubwa kuhakikisha kuwa nasafisha jina langu, kutokana na hali ilivyo kwa sasa, sitatoa taarifa nyingine yoyote ile kwenye vyombo vya habari," alisema nyota huyo.

Paqueta anaruhusiwa kuendelea kuitumikia timu yake mpaka kesi hiyo itakapomalizika na hukumu kutolewa jambo ambalo linaweza kuchukua miezi kadhaa.

Kiungo huyo panga pangua kwenye kikosi cha Brazil anaruhusiwa kuitumikia timu hiyo kwenye michuano ya Copa America, pamoja na kwamba alipumzishwa kwa muda mrefu lakini akacheza kwenye mchezo dhidi ya England uliopigwa kwenye Uwanja wa Wembley Machi mwaka huu.

Paqueta alipewa kadi kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Leicester katika dakika ya 60 baada ya kumfanyia madhambi Boubakary Soumare, akapewa dhidi ya Villa kwa kumchezea madhambi John McGinn dakika ya 70 na dhidi ya Leeds katika dakika ya 65 kwa kumvuta jezi Crysencio Summerville.

Paqueta alipewa kadi yake ya mwisho msimu huu dhidi ya Bournemouth alipooushika mpira kwenye dakika za nyongeza matukio ambayo FA wanayafanyia uchunguzi.

Chanzo: Mwanaspoti