Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisa deni la Sh1.4 milioni, Wachezaji, Kiongozi Arusha FC wazuiwa hotelini

Arusha Pic Data Arusha FC

Wed, 3 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wachezaji 23 na kiongozi mmoja wa timu ya Arusha FC inayoshiriki First League (zamani Daraja la Pili) wameshindwa kuondoka katika hoteli waliyofikia jijini Mwanza kwenda mkoani Shinyanga kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao ujao wa ligi dhidi ya Kurugenzi utakaopigwa Jumamosi Mwadui Complex.

Timu hiyo ilifika jijini Mwanza Oktoba 29 kwa usafiri wa basi walilokabidhiwa na ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Arusha na kufikia katika hoteli hiyo (jina linahifadhiwa) na kesho yake (Jumamosi) ikacheza dhidi ya Copco Veteran katika Uwanja wa Nyamagana wakikubali kipigo cha mabao 2-0.

Akizungumza na Mwanaspoti leo Meneja wa timu hiyo, Omary Muhomba ambaye ni kiongozi pekee aliyebaki na timu hotelini hapo amesema wanadaiwa jumla ya Sh1.4 milioni ambazo ni gharama za kulala vyumba tisa, chai na chakula cha usiku na mchana kwa siku sita walizokaa hotelini hapo.

Muhomba amefafanua kuwa Sh 810,000 ni gharama ya kulala siku sita kwa vyumba tisa kila chumba wakilipia Sh 15,000, huku Sh 468,000 zikiwa ni gharama za chakula cha mchana na usiku na Sh 156,000 ni deni la chai.

Amesema tayari Kocha Msaidizi Abdallah Msauka aliyeiongoza kwenye mchezo dhidi ya Copco na Meneja Mkuu Charles Mwaimu wameondoka kurejea Arusha, huku akiomba Wanachama, wadau, mashabiki na viongozi wa mkoa huo kuona namna ya kunusuru hali hiyo ili timu iweze kuondoka kuelekea mkoani Arusha kwa ajili ya mchezo ujao.

Nahodha wa timu hiyo Charles Kamtwela amesema hali hiyo  inawaathiri wchezaji kisaikolojia kwani wanashindia chakula cha Sh 1,500 kwa siku licha ya kufanya mazoezi magumu, huku akisisitiza kuwa kama hali itaendelea hivyo itaathiri utendaji wa wachezaji na kukwamisha mipango ya kuirejesha timu hiyo Championship.

"Sisi wachezaji tumejitahidi kuvumilia ndiyo maana unaona hadi sasa tupo hapa nimejaribu kuwasihi wachezaji wenzangu wamenielewa, tunashindia chakula kidogo tu cha Sh 1,500 kwa mama ntilie kwahiyo tunaomba viongozi wanusuru hali hii sisi wachezaji tuko tayari kuipambania timu," amesema Kamtwela.

Arusha FC (AFC) katika michuano ya First League imeshacheza mechi tatu ikishinda mchezo mmoja wa nyumbani dhidi ya Alliance kwa mabao 2-1, ikanyang'anywa ushindi na kupewa Mbao FC baada ya mchezo wao kushindwa kufanyika na kuchapwa mabao 2-0 na Copco Veterani katika mechi ya tatu.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz