Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisa Simba, Minziro ateta na mastaa wake, wapiga tizi saa tano

Prisons TZ Saa Tano Kisa Simba, Minziro ateta na mastaa wake, wapiga tizi saa tano

Mon, 2 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tanzania Prisons leo imetumia zaidi ya saa nne kujifua kuwakabili Simba, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Fredi Felix ‘Minziro’ akitenga zaidi ya dakika 60 kufanya kikao na nyota wake kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Timu hiyo inatarajia kuwa kibaruani Alhamisi ya wiki hii kupepetana na Simba ikiwa inaburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi moja, huku Wekundu waliofuzu makundi Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa nafasi ya tatu kwa alama tisa.

Wapinzani hao wanakutana ikiwa Simba inakumbuka ushindi walioupata nje ndani msimu uliopita wakianza na ile 1-0 Sokoine kisha kuinyuka 7-1 katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam na sasa wanakutana tena kusaka heshima na visasi.

Katika mazoezi ya leo, Minziro alianza kikao na vijana wake kilichodumu kwa zaidi ya lisaa limoja kuanzia saa 4 hadi 5:37 asubuhi kisha kuendelea na mazoezi yaliyomalizika saa 9:00 mchana ikiwa ni kujiandaa dhidi ya Simba, Oktoba 5 mwaka huu.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, kocha huyo amesema matokeo waliyonayo si mazuri sana hivyo wanahitaji kurejea kwenye ubora na leo waliamua kutumia muda mrefu kusahihisha na kuboresha maeneo yote ili kushinda mchezo huo.

“Ni mechi ngumu lakini tunahitaji kushinda ili kurejesha ubora wetu, tumetumia muda mwingi kutokana na jana Jumapili hatukuwa na mazoezi hivyo nimefurahia mazoezi na tunajiandaa kwa mapambano,” amesema Minziro.

Naye Nahodha wa timu hiyo, Jumanne Elfadhiri amesema mechi na matokeo yaliyopita hawayakumbuki tena badala yake kazi na akili kubwa ni kwenye mechi dhidi ya Simba akieleza kuwa makosa yaliyoonekana, benchi la ufundi limeyarekebisha.

“Tulifanya makosa mechi zilizopita tukapoteza, lakini tumeendelea na mazoezi kwa kusahihisha makosa na tunaendelea kujiandaa dhidi ya Simba kuhakikisha tunashinda na tutakomaa na timu yote siyo kwa mchezaji mmoja,,” amesema staa huyo

Wakati huohuo, Ofisa habari wa timu hiyo, Jackson Mwafulango ametangaza viingilio katika mchezo huo ikiwa mzunguko ni Sh 5,000, huku jukwaa kuu (VIP) ikiwa ni Sh30,000, tiketi zikianza kuuzwa leo Oktoba 2 akiwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi.

Chanzo: Mwanaspoti