Uongozi wa Yanga umesema kuwa utapambana vya kutosha katika mchezo wa marudiano dhidi ya Rivers United huku wakisema hawataki yawatokee kama waliyoyatokea Simba kwa Jwaneng Galaxy.
Simba wanakumbukwa kwa kuondolewa na Jwaneng Galaxy wakiwa nyumbani katika Uwanja wa Mkapa ambapo kabla ya mchezo huo Simba walishinda mchezo wao wa ugenini nchini Botswana kwa mabao 2-0, kisha wakaja kupigwa 3-1 kwa Mkapa.
Akizungumza nasi, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kuwa katika mchezo wao dhidi ya Rivers hawataki yale yaliyojitokeza kwa Jwaneng na Simba ambao walishinda ugenini kisha wakaja kupoteza mchezo nyumbani na kutolewa jambo ambalo hawatakulbali liweze kutokea kwa Mkapa.
“Hatutaki yajitoke yale ambayo yaliwatokea Simba katika mchezo wao dhidi ya Jwaneng ambapo waliweza kushinda wakiwa ugenini kisha wakaja kupigwa mabao matatu nyumbani, sisi hatutaki hayo yaweze kujitokeza.
“Najua kwenye mpira lolote huweza kujitokeza lakini kwa namna moja ama nyingine lazima tuhakikishe kuwa mechi inaisha mapema kwenye Uwanja wa Mkapa jambo ambalo ni lazima wachezaji wetu watambue kuwa wanatakiwa kupambana kuipa timu matokeo ya ushindi na tuweze kuandika historia ya kutinga nusu fainali,” alisema Kamwe.