Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisa Onana kurejea Man United, Ten Hag meno yote nje

Ten Hag X Onana Kisa Onana kurejea Man United, Ten Hag meno yote nje

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yaani mambo ni yaleyale na hakuna cha afadhali wala nini, lakini unaambiwa kocha wa Manchester United, Erik ten Hag amefurahishwa na kurejea kwa kipa wake Andre Onana baada ya Cameroon kutolewa katika hatua ya 16-Bora ya Afcon.

Jambo la kujiuliza anafurahi nini ilhali Onana si lolote si chochote katika kikosi hicho cha Mashetani Wekundu wa Old Trafford? Habari ikufikie kwamba Tena Hag humwambii kitu kwa kitu huyo anayeongoza kwa maboko katika mechi nyingi alizodakia chama hilo tangu alipotua msimu huu akitokea Inter Milan.

Jana pia kipa anayesaidiana na Onana, Mturuki Altay Bayındır alichomesha wakati chama lake lilipokuwa likicheza na kitimu flani cha mchangani kinachoitwa Newport County katika mchezo wa raundi ya tano wa Kombe la FA, ambapo aliruhusu mabao mawili baada ya chama lake kuongoza kwa mabao mawili.

Hata hivyo, ponapona ya Mashetani Wekundu ilikuja pale Anthony na Rasmus Hojlund walipofunga mabao mawili kipindi kile cha pili na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa Man United kushinda 4-2.

Tukirejea katika ishu ya Onana ambaye timu yake ilimkodishia ndege ili kuwahi michuano ya Afcon kwa gharam ya Sh250 milioni ambako pia alichomesha mechi ya kwanza kabla ya kutupwa benchi iliyofuata, Ten Hag anakenua kwa sababu nyanda huyo kipenzi anarudi mzigoni.

Cameroon ilifuzu hatua ya mtoano ya Afcon, lakini ilikwama mikononi mwa Nigeria katika hatua ya 16 –Bora ikilala kwa mabao 2-0 shukrani kwa mabao ya supastaa wa Atalanta ya Ligi Kuu ya Italia, Ademola Lookman.

Kipa huyo namba moja wa Manchester United alicheza mechi moja tu ambayo walilala 3-1 dhidi ya mabingwa watetezi Senegal ikiwa ni mechi yao ya pili ya hatua ya makundi na tangu hapo kocha Rigobert Song akamtema kikosini. 

Akizungumza kabla ya kipigo cha 16-Bora, kocha wa Cameroon, Rigobert Song amebainisha kwamba alilazimika kufanya mabadiliko ya kumtema Onana baada ya timu yake kuruhusu mabao sita katika hatua ya makundi.

Baada ya timu yake kutolewa Afcon, Onana sasa anajiandaa kurejea Manchester United, huku Ten Hag akithibitisha anatarajia namba moja wake arejee kabla ya Alhamisi.

"Andre Onana atarejea kwa ajili ya kuwa hapa Alhamisi. Pengine, kwa mara ya kwanza nikiwa kocha hapa, naweza kuchagua kikosi imara zaidi," amesema kocha huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live