Mashabiki wa Manchester United wanamshinikiza Erik ten Hag amcheze Scott McTominay nafasi ya fowadi badala ya Wout Weghorst baada ya kiungo huyo kupachika mabao mawili dhidi ya Hispania.
Kiungo huyo alikuwa kinara kwenye mchezo wao wa kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Ulaya (EURO 2024) baada kuisaidia Scotland na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, vile vile McTominay akacheka na nyavu mara mbili tena dhidi ya Cyprus kwenye ushindi wa mabao 3-0.
Sasa mashabiki wa Man United wameibuka wakidai Mctominay ndio anastahili kucheza nafasi ya fowadi kutokana uwezo wake wa kupachika mabao aliyoonyesha kwenye mechi za kimataifa.
Kwa upande wa Weghorst amekuwa kichekesho cha mashabiki wa soka baada ya kushindwa kung'ara kwenye mechi zao za kufuzu michuano ya Euro ambayo yatafanyika mwakani Ujerumani ikiwa mwenyeji.
Mashabiki walimuona kituko baada ya kushindwa kufunga hata dhidi ya wachezaji 10 wa Gibraltar, huku beki Nathan Ake akifunga mara mbili katika mchezo huo. Licha ya kuzingua kwenye mchezo huo Uholanzi ilishinda mabao 3-0 katika mchezo huo uliyochezwa Rotterdam.
Shabiki mmoja wa Man United alizungumza kupitia mtandaoni akidai "Mctominay amefanya kazi kubwa sana katika mechi za kimataifa zaidi ya Weghorst".
Mwingine akaandika: "Mctominay ana kitu anakitengeneza, mabao mawili dhidi ya Hispania sio mchezo," Shabiki wa tatu akamaliza kwa kusema "Mctominay anastahili kuwa fowadi badala ya Weghorst nadhani Ten Hag angempanga katika mechi hizi zilizobaki,"
Weghorst amefunga mabao mawili tu katika mechi 28 alizocheza msimu huu tangu alipotua mkopo akitokea Burnley.