Nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk anadaiwa kuwa tayari kusaini mkataba mpya wa kuitumikia hadi 2026.
Van Dijk ambaye amepokea ofa kadhaa za Uarabuni wakati huu ambapo mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu, anadaiwa kuwa na nia ya kuichezea Liverpool hadi atakapomaliza Kombe la Dunia 2026 ndipo aondoke.
Beki huyo wa kimataifa wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 33, ni miongoni mwa mastaa tegemeo katika kikosi cha Liverpool kwa sasa.
Licha ya kutaka kubaki Liverpool italazimika kumpa mshahara mnono tofauti na ule ambao anaupokea kwa sasa. Van Dijk anaamini akiondoka na kwenda Uarabuni huenda asiitwe kuitumikia Uholanzi katika Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani. Mbali ya Van Dijk, beki mwingine tegemeo anayehusishwa kuondoka ni Trent Alexander Arnold ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
LICHA ya taarifa za hivi karibuni kufichua beki wa kulia wa Newcastle United na England, Kieran Trippier, 33, hataondoka kwenye timu hiyo, taarifa mpya zinaeleza amewasiliana na mabosi wa Newcastle kuwaambia anataka kuondoka. Kwa sasa anaweza akatimkia Uturuki ambako Jose Mourinho na Fenerbahce yake wanamhitaji na pia Besiktas inammezea mate.
MEMPHIS Depay ambaye yupo huru tangu aachane na Atletico Madrid katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi amefaulu vipimo vya afya na anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Corinthians ya Brazil. Timu mbalimbali zilitaka kumsajili staa huyu wa kimataifa wa Uholanzi lakini wababe hao wa Brazil waliweka pesa nyingi.
MANCHESTER United na Newcastle United zinapambana jino kwa jino kuiwania huduma ya kiungo wa zamani wa Juventus, Adrien Rabiot ambaye yupo huru. Katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana Man United ilijaribu kumsajili lakini ilishindikana. Staa huyu wa kimataifa wa Ufaransa alionyesha kiwango bora katika Euro mwaka huu.
ATLETICO Madrid, Barcelona na Juventus ni miongoni mwa timu zinazotaka huduma ya kiungo wa Arsenal na Ghana, Thomas Partey ambaye mabosi wa Arsenal wanadaiwa kuwa tayari kumuuza ikiwa itapatikana timu itakayotoa ofa nzuri. Benchi la ufundi la Arsenal lipo tayari kuachana na Partey kutokana na majeraha yake ya mara kwa mara anayoyapata.
PARIS St-Germain ni miongoni mwa timu zilizoonyesha nia ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Salah amekuwa akihusishwa na dili za Uarabuni lakini hivi karibuni matajiri kutoka Ufaransa wameanza kumnyemelea ili akazibe pengo la Kylian Mbappe.
ARSENAL imeripotiwa kuwa haina mpango wa kumwachia kiungo raia wa Italia, Jorginho licha ya timu mbalimbali ikiwemo Galatasaray ya Uturuki kuonyesha nia ya kutaka kumsajili katika dirisha hili. Jorginho anahusishwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Arsenal. Galatasaray inataka kukamilisha usajili wake hata kwa mkopo.
BARCELONA inaangalia uwezekano wa kumsajili beki wa Bayer Leverkusen, Jonathan Tah, 28, katika dirisha lijalo la majira ya baridi au mwisho wa msimu baada ya staa huyo kuthibitisha kuwa hana mpango wa kuendelea kusalia Leverkusen msimu ujao ambapo mkataba wake utakuwa umeshamalizika. Katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi Tah alikuwa akiwindwa na Bayern Munich.