Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisa Azam FC, Gamondi awaita fasta Aziz Ki, Aucho

Aucho Aziz Ki Kisa Azam FC, Gamondi awaita fasta Aziz Ki, Aucho

Mon, 16 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya Bodi ya Ligi kufanya marekebisho ya ratiba kiujumla katika Ligi Kuu, kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amefanya mawasiliano ya haraka na mastaa wake Stephane Aziz Ki, Khalid Aucho na Djigui Diara na kuwataka warejee haraka baada ya majukumu yao ya timu za Taifa na kuingia kambini kwa ajili ya mchezo wao ujao dhidi ya Azam FC.

Ki, Aucho na Diara wapo katika timu zao za taifa na watacheza mechi zao za kirafiki za kalenda ya Fifa, Oktoba 18 katika viwanja tofauti na kocha huyo amewataka wageuze Oktoba 19 ili kuwahi mechi yao ijayo.

Awali, Yanga na Azam Fc zilikuwa zicheze Oktoba 25 lakini mabadiliko hayo yatafanya timu hizo zikutane Oktoba 22.

Gamondi alisema kitendo cha ratiba ya Ligi Kuu kubadilika kwake ni kicheko kwa sababu ana imani kubwa wachezaji wake hao watakuwa wamepata dakika nyingi za kucheza katika timu zao za Taifa na kupata utimamu wa mwili ambao utawasaidia katika mechi yao dhidi ya Azam FC.

“Djigui (Diara), Stephane (Aziz Ki) na Khalid (Aucho) wanacheza mechi zao za mwisho za kirafiki wakitumikia timu zao za taifa Oktoba 18 nimewaambia warudi siku inayofuata ili kujiandaa na mchezo ulio mbele yetu;

“Nimefurahishwa na mabadiliko ya ratiba kwani nilikuwa naumiza kichwa namna ya kupata mechi ya kirafiki ili kuwajenga kimwili na kiushindani wachezaji wangu ambao wamekaa nje ya uwanja kwa muda bila kucheza.”

Akizungumzia maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Azam FC, alisema wachezaji wote walishaingia kambini isipokuwa baadhi ambao wameitwa kuzitumikia timu zao za taifa huku akisisitiza anahitaji muendelezo wa ubora na ushindani kikosini kwake.

“Ni wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza wameitwa kwenye timu zao za taifa hilo haliondoi mimi kuendelea kuwaandaa wachezaji waliopo na wao pia wana mchango kwenye timu;

“Yanga haimtegemei mchezaji mmoja, wote wanategemeana hivyo kurudi kwa wachezaji ni mwanzo mzuri wa kuwaandaa tayari kwaajili ya mchezo ulio mbele yetu, hautokuwa rahisi tunakutana na timu ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja, hicho ni kipimo sahihi cha mechi za ushindani.”

Yanga ikimalizana na Azam FC Oktoba 25 itakuwa na kibarua kingine dhidi ya Singida Big Stars Oktoba 28 na Novemba 8 itavaana na watani wao Simba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live