Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisa Amrouche, CAF yaipiga rungu TFF

Wallace Karia Bila Vijana Rais wa TFF, Wallace Karia

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limetoza kiasi cha Dola 10,000 (Sh25 milioni) kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na uvunjaji wa maadili uliofanywa na kocha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Adel Amrouche hivi karibuni uliosababisha kocha huyo apewe adhabu ya kufungiwa mechi nane.

TFF imetozwa fedha hizo kutokana na kuvunja kanuni ya 110 ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) inayotaka timu shiriki kudhibiti mwenendo wa ofisa/maofisa wake.

“Chama shiriki kinapaswa kuwajibika kwa tabia za wahusika wa msafara wake (maofisa na wachezaji) katika kipindi chote hadi mwisho wa shindano,” inafafanua kanuni hiyo.

Adhabu hiyo ya Tanzania, imetolewa sambamba na ile ambayo Amrouche alipewa na bodi ya nidhamu ya Caf baada ya kutoa kauli ya tuhuma kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Morocco (FRMF) kuwa limekuwa likifanya vitendo vya hujuma kwa timu pinzani.

“Morocco inaamua kila kitu katika soka la Afrika. Pia wanachagua waamuzi wao. Tunabaki kuwa watazamaji kwa sababu wanaamua kila kitu. Sitashangaa yakijirudia haya katika mchezo ujao wa Afcon dhidi yao,” alinukuliwa Amrouche aliyeajiriwa Machi, mwaka jana kuchukua nafasi ya Kim Poulsen.

Hata hivyo, siku moja baadaye, Rais wa TFF, Wallace Karia alijitokeza hadharani na kutangaza msimamo wa shirikisho kuwa hausapoti kauli ya kocha huyo na kauli aliyotoa ni yake binafsi.

“Sisi kama TFF hatukubaliani na hiyo kauli. Shirikisho la Morocco na Tanzania ni marafiki tuko mbali na kauli zake na hatukubali. Tutajua tutafanya nini, tuko kwenye mashindano,” alisema Karia.

Katika hali ya kushangaza, mara baada ya mchezo ambao Tanzania ilipoteza kwa mabao 3-0, Amrouche aliwasifia Morocco alisema wana timu nzuri na bora.

“Mbinu yetu ya mchezo ilifeli. Hatukutarajia matukio haya lakini nawapongeza Morocco kwa kiwango walichoonyesha na matokeo waliyopata. Ubora wa wachezaji wa Morocco ulileta tofauti kubwa na walistahili kushinda.

“Tulitaka matokeo mazuri lakini pia nilikuwa na majeruhi wengi sana jambo ambalo lilituathiri. Kisha tukafanya na makosa binafsi,” alifafanua Amrouche.

Hata hivyo gazeti hili limebaini kwamba TFF imeshamtema Amrouche.

Chanzo: Mwanaspoti