Mkurugenzi wa Huduma za Dharura Wizara ya Afya Dk Elias Kwesi amelielekeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutowatumia watu wasio na ujuzi wa masuala ya dharura na maafa kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Dk Kwesi ameyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya huduma za afya kabla nje ya Hospitali na kukabiliana na maafa na dharura.
Mafunzo hayo yanafanyika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas) yakifadhiliwa na Shirika kutoka nchini Uturuki (TiKA) ikihuisha wataalamu zaidi ya 700 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
"Nchi yetu itakuwa mwenyeji wa AFCON 2027, niwaombe TFF vigezo vya watoa huduma wa afya kwenye mashindano vizingatiwe, tutajenga heshima yetu ngazi ya michezo"alisema.
Dk Kwesi alielekeza kuwa watu waliopata mafunzo ndio watoe huduma za dharura kwa wachezaji na siyo deiwaka.
Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Muhas, Profesa Emmanuel Balandya alisema mafunzo yaliyoanza kutolewa na chuo hicho ya masuala ya huduma za dharura na majanga ni maandalizi ya utayari wa kukabiliana na majanga.
Miongoni mwa viasharia vya uwezekano wa kutokea majanga ni mkusanyiko mkubwa wa watu, mwaka 2027 tunatarajia kuandaa mashindano ya makubwa ya AFCON na maelefu ya watu watashiriki,"alisema.