Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kirumba iko tayari kwa Dabi

CCM KIRUMBA (600 X 409) Uwanja wa CCM Kirumba

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, Lazaro Roman amesema kwa maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea uwanjani hapo ana imani kwamba mchezo wa 'Derby ya Mzizima' kati ya Simba na Azam utachezwa katika mazingira bora na ya kuvutia.

Mchezo huo utapigwa kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Ijumaa kuanzia saa 10:00 jioni ukiwa ni mchezo wa kiporo ambao awali ulipaswa kuchezwa Novemba 28, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Meneja huyo, alisema katika kuhakikisha uwanja unakuwa tayari, kukidhi vigezo na kuvutia, waliufunga kwa wiki mbili zilizopita na kusimamisha shughuli zote za kimichezo uwanjani hapo ili kurekebisha baadhi ya maeneo, ambapo walipanda nyasi sehemu zilizokuwa na vipara, kuweka mbolea na kupalilia pembezoni mwa uwanja.

"Sehemu korofi tulizopanda majani yameanza kuota na tuna wahudumu 10 wanaotusaidia kufanya usafi na mambo mengine hapa, kwa kinachofanyika tukija kufyeka kwa mara ya mwisho uwanja utapendeza na mashabiki watafurahi soka safi," alisema. Roman aliongeza, tayari Bodi ya Ligi (TPLB) na viongozi wa baadhi wa timu zinazohitaji kuutumia uwanja huo wameshakagua na kuridhishwa na kinachofanyika huku akisisitiza hadi kufikia siku ya mchezo dimba hilo litakuwa tayari kutoa burudani.

Mmoja wa wahudumu wa uwanja huo ambao Mwanaspoti liliwakuta wakisafisha kwa kupalilia nyasi, Halima Msindo, alisema wanaendelea kufanya usafi huku akiwahakikishia mashabiki wataburudika kwani wataukuta ukiwa katika mazingira safi.

Uwanja huo utaandaa mchezo huo muhimu ikiwa imepita miezi minne tangu mchezo wa mwisho wa Ligi kuchezwa dimbani hapo Oktoba 7, mwaka jana ambapo Geita Gold iliikaribisha Yanga huku kikosi hicho kikiibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0.

Chanzo: Mwanaspoti