Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Junior amefikia rekodi ya beki kisiki wa Yanga, Attohoula Yao baada ya kufikisha asisti tano kwenye ushindi wa mabao 2-1 wa timu yake dhidi ya JKT Tanzania na kuondoka na pointi tatu, juzi Jumatatu.
Azam FC sasa imefikisha pointi 28 baada ya michezo 12, huku staa huyo akindelea kuwika na aliliambia Mwanaspoti anafurahi kuwa miongoni mwa wanaochangia timu kupata matokeo huku akikiri ameanza kuzoea ligi.
“Jana nimehusika kwenye ushindi wa pointi tatu baada ya kutoa pasi ya mwisho iliyozaa bao la ushindi. Nimefurahi na inaendelea kunipa picha ya namna natakiwa kucheza ili kuwa mchezaji muhimu kikosini japo siyo rahisi, inahitaji kupambana;
“Azam FC imeimarika, tunapambana kuhakikisha tunafikia malengo kwa kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa msimu ujao japo inahitajika nguvu ya ziada kutokana na ushindani mkubwa uliopo,” alisema.
Kipre alisema anafurahia maisha ndani ya timu hiyo kutokana na namna ameanza kuingia kwenye mfumo,baada ya kuanza kuelewana na wachezaji wenzake, huku akisisitiza ligi bado ngumu na wana mechi nyingi, hivyo wanatakiwa kuendeleza juhudi zao ili kujikusanyia pointi zitakazowafanya watimize malengo.
“Ligi ni ngumu, timu nyingi zinapambana kupata matokeo, juhudi binafsi za mchezaji mmoja mmoja na mbinu za benchi la ufundi zikitumika kama inavyotakiwa ni rahisi kufikia malengo;
“Nafurahi kucheza na kila mchezaji aliyepo Azam FC, usajili wake ndani ya timu una maana kubwa, hivyo ili kujenga timu bora na ya ushindani ni kutakiwa kukubali kupewa maelekezo bila kujali nani anakuelekeza, lengo ni moja kucheza mashindano ya kimataifa msimu ujao,” alisema.