Makamu wa Rais wa Klabu ya Yanga, Arafat Haji amevunja ukimya baada ya Yanga Princess kutoanza vyema kwenye Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) na ametaja sababu, huku akiwataka mashabiki watulie kwani timu bado inatengenezwa.
Yanga iko nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na imecheza mechi sita ikifungwa tatu dhidi ya Simba Queens 3-1, JKT Queens 3-1 na kufungwa bao 1-0 na Ceasiaa Queens.
Kiongozi huyo ameandika ujumbe huo kwenye ukurasa wa mitandao ya kijamii, timu hiyo inaendelea kuboreshwa ndani na nje ya uwanja.
"Wananchi timu yetu ya Yanga Princess licha ya kukosa ushindi kwenye baadhi ya mechi zilizopita hususani Ligi Kuu ya Wanawake, imeendelea kuimarika tofauti na ilipotoka."
"Yanga Princess bado inaendelea kufanyiwa maboresho ya kiufundi kwenye maeneo kadhaa, kuanzia ndani hadi nje uwanja, tutakubaliana kwa pamoja, ilipo leo Yanga Princess sio ilipokuwa misimu kadhaa nyuma, taratibu mabadiliko yanaendelea kufanyika na maendeleo yanaonekana."
"Wakati maboresho yanaanza kufanyika kwenye timu yetu ya wanaume tulikuwa tunapiga hatua moja baada ya nyingine na leo tupo juu kabisa kwenye soka la Tanzania, Afrika Mashariki na Kati na Afrika nzima, mabadiliko yanapofanyika matokeo hayaonekani ama hayaji kama unavyoweka sukari kwenye chai au kuwasha swichi na taa ikawaka papo-hapo badala yake ni mchakato unahitaji muda,
Kinachotengenezwa na kuandaliwa ndani ya Yanga Princess matokeo yake yataanza kuonekana muda si mrefu, kila Mwananchi ataanza kusherehekea mafanikio ya timu hii,viongozi wenu tunaendelea kufanya kila linalo wezekana kuhakikisha timu yetu inafikia malengo tuliyojiwekea," ameandika Arafat.