Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kipigo cha Al Merrikh muhimu leo chamvuruga Gomes

951d93d14ffb5abd60ee49c9081de4e6 Kipigo cha Al Merrikh muhimu leo chamvuruga Gomes

Wed, 3 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA Mkuu wa klabu ya soka ya Simba, Didier Gomes amesema mchezo wao unaofuata wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan hautakuwa rahisi kutokana na wapinzani wao kupoteza mechi mbili mfululizo.

Simba juzi iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, matokeo ambayo yaliifanya kuzidi kuwasogelea vinara Yanga kwa kufikisha pointi 45, lakini pia ikizidi kujiimarisha kabla ya mechi hiyo ya kimataifa itakayochezwa Khartoum, Sudan mwishoni mwa wiki hii.

Kocha huyo raia wa Ufaransa alizungumza na vyombo vya habari baada ya mchezo na JKT Tanzania kumalizika na kueleza kuwa pamoja na ugumu waliokutana nao kwenye mchezo huo, lakini alilazimika kufanya mabadiliko machache kwenye kikosi chake kutokana na kuupa uzito mkubwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Merrikh.

“Tuna mechi ngumu ya Ligi ya Mabingwa siku tano zijazo hivyo ilikuwa lazima baadhi ya wachezaji niwapumzishe kwa ajili ya kuweka nguvu kwenye mchezo wetu ujao ambao tutacheza ugenini na timu nzuri licha ya kupoteza mechi mbili hivi karibuni, naamini hawatokubali kuendelea kupoteza nyumbani,” alisema.

Gomes alisema ushindi dhidi ya JKT Tanzania umezidi kumpa matumaini ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kuitoa Yanga kileleni mwa msimamo na kilichomfurahisha zaidi ni kiwango bora kilichooneshwa na wachezaji wake katika mchezo huo.

Alisema kupata mabao mawili ya haraka kwenye kipindi cha kwanza iliwasaidia kucheza bila presha huku wakiwaachia wapinzani wao kazi ya kusawazisha ndio sababu akaamua kuwatoa baadhi ya wachezaji ili kuepuka majeraha.

Kwa upande wake, kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohamed ‘Bares’ alisema vijana wake walizidiwa kimbinu na wapinzani wao Simba jambo lililosababisha safu yake ya ulinzi kuruhusu mabao mepesi kwenye dakika za mwanzoni za mchezo huo.

“Nakubali tulishindwa kuwadhibiti Simba na kujikuta tunaruhusu mabao mawili ya mapema ambayo yalitokana na uzembe wa mabeki wangu, lakini nawapongeza pia vijana wangu kipindi cha pili walijipanga na kucheza vizuri ingawa hatukufanikiwa kufunga bao,” alisema Bares.

Matokeo ya juzi yanaifanya Simba kusaliwa na mechi mbili za viporo kufikia mechi ilizocheza Yanga ambayo ndio kinara hivi sasa ikikusanya pointi 49 kwa kucheza michezo 21, wakati Simba imecheza mechi 19 na kukusanya pointi 45.

Chanzo: habarileo.co.tz