Wawakilishi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kutoka visiwani Zanzibar, Kipanga FC kitawafuata wapinzani wao Club Africain ya Tunisia kesho Alhamisi huku Kocha Mkuu, Hassan Abdulrahman Said akitamba kufanya vizuri mechi hiyo ya marudiano.
Katika mchezo wa awali timu hizo zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja ambapo sasa Kipanga wana kazi ya kutafuta ushindi ugenini, mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Stade Olympique de Rades, Oktoba 16 mwaka huu.
Kocha huyo alisema; “Tumerejea mazoezini, tumejifunza mechi tuliyocheza nyumbani na tunajipanga kwenda kufanya vizuri kwa kurekebisha makosa yaliyotokea na mazuri kuyaboresha katika mechi ya juzi ili tufanye vizuri mechi hiyo.” Kuhusu safari yao, alisema kikosi cha watu 35 kitaondoka Alhamisi kikiwa na wachezaji, viongozi wa timu hiyo na Waandishi wa Habari na mashabiki kwa ajili ya kuwapa sapoti.
“Sisi tunaenda siku tatu kabla kuzoea mazingira na tufanyaje mazoezi siku mbili kuzoea uwanja ikiwa ndo mara yetu ya kwanza kwenda Tunisia.”