Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kipa ayakataa mabao ya Aziz Ki

Aziz Ki.png Aziz Ki

Thu, 5 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Said Mohammed ‘Nduda’ amesema licha ya frikiki za Stephan Aziz KI kuwa za kiwango lakini ni uzembe wa kipa kufungwa.

Aziz Ki, aliifungia Yanga bao pekee kwa mpira wa adhabu ambao kipa wa Mtibwa Sugar, Razack Shekimweri alishindwa kuudaka ukiwa ni muendelezo wa kufunga mabao ya aina hiyo.

Pia, alisababisha bao la faulo katika mchezo dhidi ya Azam dhidi ya kipa Ali Ahamada, na awali alifunga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba langoni akiwa Aishi Manula.

Nduda ambaye amewahi kuidakia Mtibwa Sugar, alisema ni uzembe uliopitiliza wa kipa kuruhusu mpira udunde mbele yake kwani ni lazima utampoteza maboya.

“Ukidunda hata ufanyaje huwezi kuudaka ninachokiona yale ni mabao rahisi sana na kipa ukifungwa lazima ujitafakari,” alisema Nduda ambaye ameichezea CDA ya Dodoma na Timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ na Yanga.

Kipa huyo aliwashauri makipa kuwa na utaratibu wa kupanga mabeki warefu mwanzo wa ukuta ili kumfanya mpigaji ashindwe kuupitisha mpira.

“Mchezaji wa kwanza katika ukuta kulia ama kushoto ni lazima awe mrefu lakini kipa chungulia ukuta wako kabla mpira haujapigwa, makipa wengi hawafanyi hivyo ndio maana wanafungwa mabao ya kizembe,”alisema.

Hata hivyo, ameiangalia Ligi Kuu msimu huu na kudai ina ubora kutokana na timu nyingi kujipanga.

Chanzo: Mwanaspoti