Achana na ushindi wa Yanga juzi, unaambiwa kipa wa Tanzania Prisons, Benedict Haule hawezi kumsahau kiungo Feisal Salum aliyemhangaisha kwa mishuti yake ya mbali na kumnyima raha golini.
Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini hapa na kuendelea kukaa kileleni kwa alama 23.
Akizungumza na Mwanaspoti, Haule alisema tangu akutane na Yanga katika michezo mitatu ndio mara ya kwanza kufungwa na timu hiyo kongwe nchini.
Alisema mbali na kumchafulia rekodi yake safi, lakini miongoni mwa wachezaji waliompa hekaheka golini ni Feisal Salum ambaye alionekana kutawala zaidi eneo la katikati.
“Hawakutuzidi sana, ilikuwa ni bahati yao tu, lakini Fei alikuwa bora kwa sababu pale kati alipamudu sana, hata mashuti yake mengi yalinihangaisha,” alisema Haule.
Kipa huyo ambaye anaichezea timu hiyo kwa mkopo kutokea Azam Fc, alisema bado wana matumaini ya kuweza kufanya vizuri kwenye michezo inayofuata dhidi ya Geita Gold na Kagera Sugar kwani kikosi kipo fiti.
Alisema kwa sasa akili na nguvu zao zinaelekezwa kwenye mechi hizo za ugenini ili kurekebisha makosa yao kurudi na pointi sita kupanda nafasi za juu.
“Hatuwezi kukata tamaa kwa sababu bado mechi hazijaisha hivyo tunajipanga na michezo ijayo tukianza na Geita Gold kisha Kagera Sugar,” alisema Haule.