Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kipa Pamba aliyelelewa Yanga SC

Rakim Sheikh Rahim Sheikh

Sat, 11 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni mmoja wa makipa wanaofanya vizuri kwa sasa katika Ligi ya Championship kutokana na uzoefu mkubwa aliouchota kwenye Ligi Kuu akiwa na umri mdogo.

Rahim Sheikh ambapo amedaka mechi zote tisa za timu yake ya Pamba Jiji FC akiruhusu mabao matano huku akiwa na cleansheet nne akiisaidia timu hiyo kukamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa mashindano hayo.

Kipa huyo aliyejiunga na Pamba Jiji ya Mwanza mwanzoni mwa msimu huu ni mzaliwa wa Temeke jijini Dar es Salaam akitokea familia ya soka akiwa ni mtoto wa tatu kati ya watano wa mzee, Sheikh Abdallah ambaye ni kipa wa zamani wa Pan Africans na Red Star za jijini Dar es Salaam huku pia akizinoa timu za Ashanti United na Manyema FC.

Kinda huyo mwenye uwezo mkubwa langoni amekuwa na safari ya mafanikio katika soka nchini tangu alipotambulika mwaka 2017 kutoka Yanga kisha Arusha FC, Mbao ya Mwanza, KMC ya Dar es Salaam na Dodoma Jiji.

Mwanaspoti lilizungumza na kipa huyo ambaye amefunguka mengi ikiwamo maumivu ya kushuka daraja na Mbao FC, mchezo wake wa kwanza Ligi Kuu, ushindani wa namba ulivyomkimbiza Yanga na namna ambavyo kucheza timu moja na makipa wakubwa kama Juma Kaseja, Shaban Kado na Metacha Mnata vimemkomaza zaidi kisoka.

DIDA, KAKOLANYA WAMKIMBIZA YANGA

Rahim ambaye aliamua kufuata nyayo za baba yake mzazi kuwa kipa, anasema safari yake ya soka ilianzia katika timu ya vijana ya Yanga (U20) kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa msimu wa mwaka 2017/2018 lakini ushindani mkali wa namba ukamkimbiza mbele ya Deogratius Munishi ‘Dida’, Ally Mustapha ‘Barthez’ na Beno Kakolanya.

“Maisha yangu ya soka yalianzia timu ya vijana Yanga ya U20 na kupandishwa timu kubwa niliwakuta makipa Dida, Barthez, Kakolanya baadaye wakaondoka wakaja kina Ramadhan Kabwili na Youthe Rostand ambao pia walinikuta lakini mwaka 2018 niliondoka nikaenda Arusha United nikacheza nusu msimu ndipo nikasajiliwa Mbao FC,” anasema Rahim.

KMC, DODOMA JIJI

Akiwa na Mbao FC ya Mwanza kuanzia mwaka 2018 hadi 2020, Rahim alicheza kwa kiwango kikubwa ambapo msimu wa 2019/2020 mzunguko wa pili Ligi Kuu alicheza mechi nne bila kuruhusu bao. Kiwango chake kikazivutia timu nyingi lakini akatua KMC na baadaye Dodoma Jiji.

“Timu ambayo naikumbuka sana ni Mbao kwa sababu nilicheza mechi nyingi za Ligi Kuu, nilivyofika KMC nilicheza mechi nne za kwanza tukashinda tatu na kupoteza moja timu ikaongoza ligi kwa muda huo.

“Nikaitwa timu ya taifa ya vijana niliporudi nikawa nimepoteza nafasi ya kwanza kwahiyo nikawa na changamoto ya namba na kupata muda wa kucheza kwa sababu makipa wote waliokuwapo walikuwa wazuri,” anasema Rahim.

ANACHOTA UJUZI KWA BABA

“Nimezaliwa katika familia ya mpira, baba yangu (Sheikh Abdallah) alikuwa mchezaji wa zamani, alicheza Pan African na Red Star nafasi ya kipa, baadaye akawa kocha akizifundisha Ashanti na Manyema FC, kwahiyo nilichagua nafasi ya kipa kwa sababu ya mzee wangu,” anasema.

“Baba yangu ni mwalimu mkubwa kwanza kila muda hachoki kunielekeza kipa anatakiwa kufanya nini akiwa kwenye kiwanja cha mazoezi na mechi. Muda mwingi huniambia mambo ya ufundi na majukumu ya kipa ni yapi kwahiyo najivunia sawa uwepo wake.”

KADO NI FUNDI

Rahim amedaka mechi zote tisa za ligi za timu yake ya Pamba mbele ya kipa mzoefu nchini, Shaban Kado, ambapo kinda huyo anasema uwepo wa mkongwe huyo umemsaidia kiufundi, kupata uzoefu na kuimarika kila wakati.

“Kado ameongeza kitu kikubwa kuna mambo ambayo nilikuwa sijui nimeyajua kupitia yeye pia kuna mambo nilikuwa nadhani niko sahihi kumbe nilikuwa nakosea, kuja kwake amenifunza mengi na kujua vitu vingi ikiwamo kutokuwa na hofu nikiwa langoni,” anasema.

KASEJA, MANULA NOMA

Kipa huyo anasema anawakubali makipa na wachezaji wengi ndani na nje ya nchi lakini Juma Kaseja, Aishi Manula, Ally Salim, Abdultwalib Mshery na Shaban Kado ni miongoni mwa anaovutiwa nao zaidi wakiwa kwenye majukumu yao kwani wanakuwa na umakini na kutimiza kile kilicho mbele yao kwa usahihi.

MBAO KUSHUKA DARAJA

Rahim anaamini wakati wake mzuri kwenye soka mpaka sasa ni akiwa Mbao FC na tukio la furaha ambalo analikumbuka ni mechi yake ya kwanza langoni Ligi Kuu, huku timu ya Mbao FC kushuka daraja katika mchezo wa mtoano dhidi ya Ihefu akiwa langoni likiwa la huzuni kwake.

“Nakumbuka zaidi mechi yangu ya kwanza ya Ligi Kuu nikiwa nimetokea sub (akiba) na kuwa man of the match (mchezaji bora wa mchezo) kati ya Mbao na Singida. Lakini jambo ambalo limeniumiza sana ni mechi ya mwisho ya play off dhidi ya Ihefu tukashuka daraja.

“Niliumia sana kwa sababu malengo yangu yalikuwa makubwa baada ya kucheza mechi 11 nilifugwa mechi tatu tu kwahiyo niliumia pia viongozi walikuwa hawana cha kusema ila walitupa pole,” anasema Rahim

CHAMPIONSHIP USIPIME

Rahim ameisaidia Pamba kushinda michezo mitano ya Championship, wakipoteza mmoja pekee dhidi ya Stand United na sare tatu ambapo wamevuna pointi 18 na kukamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo huku wakifunga mabao 13 na kuruhusu matano.

Sheikh anasema mashindano hayo ni magumu na ushindani ni mkubwa kwa timu zote kwani hakuna mechi nyepesi kwa sababu timu zote 16 zina wachezaji bora, makocha na uongozi mzuri, ambapo ushindani huo unawapa Pamba hamasa ya kuendelea kupambana kufikia malengo ya kupanda daraja.

MALENGO, MUIGIZAJI

Nyota huyo anasema malengo yake ni kuendelea kucheza kwenye kiwango kikubwa ili kuwa miongoni mwa makipa wakubwa nchini na kufuata nyayo za Juma Kaseja, Aishi Manula na wengine, huku akidai kama isingekuwa soka basi angekuwa muigizaji kwani ni kazi anayoipenda sana.

“Ndoto zangu kwa sasa ni kufika malengo ambayo nimejiwekea pia kuwa kipa mkubwa mwenye mafanikio katika kazi yangu. Kama nisingekuwa nacheza mpira ningekuwa naigiza kwa sababu ni kitu ninachokipenda sana,” anasema Rahim.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: