Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kindoki ampisha Mkongo Yanga

69262 Kindoki+pic

Thu, 1 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Kipa wa Yanga Klause Kindoki amesema yuko tayari kuondoka endapo atalipwa stahiki zake zote baada ya klabu hiyo kumsajili mshambuliaji kutoka DR Congo Molinga David.

Akizungumza jana, Kindoki raia wa DR Congo alisema amesikia taarifa za jina lake kukatwa kutokana na ongezeko la idadi ya wachezaji wa kigeni.

Hivi karibuni Yanga ilikamilisha usajili wa kipa namba mbili wa timu ya taifa ya Kenya, Farouk Shikalo akitokea Gor Mahia.

Mbali na Shikalo, wachezaji wengine wa kigeni ni Patrick Sibomana, Issa Bigirimana, Sadney Khoetage, Lamine Moro, Maybin Kalengo, Papy Tshishimbi, Juma Balinya, Moringa David na Mustapha Selemani.

Ujio wa mshambuliaji mpya David Molinga raia wa DR Congo unafanya idadi ya wachezaji wa kigeni Yanga kufikia 11, hivyo jina moja lazima likatwe ili kubaki 10 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni.

Akizungumza kwa kujiamini, Kindoki alisema hatashangaa akikatwa na klabu hiyo kwa kuwa taarifa hizo amezisikia muda mrefu.

Pia Soma

Kindoki alisema anaamini bado ni kipa mwenye kiwango bora, lakini kama Yanga inataka kumuacha impe haki zake na malipo yote anayodai ili aondoke kwa amani.

“Nasikia kelele nyingi Kindoki unaachwa na Yanga, watu wananipigia simu ila mimi sijajua chochote haya mambo yananiumiza, kelele za kuachwa zinanikera ni bora niondoke kama wanataka kuniacha wanipe fedha ninazodai zote niondoke,” alisema Kindoki.

Kipa huyo alisema endapo Yanga inataka kumuacha inatakiwa kumpa taarifa mapema ili ajipange kujiunga na klabu nyingine akidai yeye si mchezaji wa kukosa timu ya kucheza msimu ujao.

“Kuna wakati nilisikia wanataka kunitoa kwa mkopo nikashangaa sana, mimi Kindoki ni kipa wa kutolewa kwa mkopo?Wafanye hayo maamuzi sasa wanipe haki zangu na barua ya kuniacha ili niondoke sitakosa timu,” alisema Kindoki.

Mmoja wa vigogo wa Yanga ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, alidai Kindoki atampisha Shikalo na tayari wamekubaliana ndani ya klabu hiyo.

“Kindoki tutamuacha si kwasababu ni kipa mbaya, hatuwezi kuwa na makipa wawili wa kigeni tayari tuna Shikalo (Farouk) pia tumemsajili Metacha (Mnata) na tuna Kabwili(Ramadhani),”alisema kigogo huyo.

Zahera alipotafutwa kuzungumzia uamuzi huo, alijibu kwa kifupi suala hilo linaendelea kujadiliwa na uongozi.

“Ndiyo, amefika Molinga unataka kujua nani ataachwa? Uamuzi huo utatoka baadaye hapa sina jibu,” alisema Zahera kwa kifupi.

Kindoki alijiunga na Yanga kwenye usajili wa dirisha kubwa Julai, mwaka 2017 akichukua nafasi ya Mcameroon, Youthe Rostand.

Chanzo: mwananchi.co.tz