Meneja wa habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amesema kuwa kinachowatisha Al Ahly kucheza na Simba ni pamoja na viungo wake wanne wa kati ambao Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, Babacar Sarr na Mzamiru Yassin.
Ahmed amesema hayo kuelekea mchezo wao wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Ahly utakaopigwa Machi 29, 2024 katika Dimba la Mkapa.
“Huyu Aliou Dieng ni mashine kweli kweli kijana kutoka Mali lakini mara zote ambazo anacheza na Simba huwa anatepeta pale kati kati kwa sababu anakutana na mashine zingine za maana, pale kati kati kuna Sadio Kanoute na ameshapona.
“Anakutana na Fabrice Ngoma ambaye hajaanza leo kukabana na Dieng ,amemkalisha sana kwenye mechi za Al Ahly na Raja Casablanca ni katika wale viumbe wa ajabu.
“Dieng anamfahamu vizuri Muzamir Yassin, bado kuna Babacar Sarr mashine mpya hiyo, hajawahi kukutana nayo. Wamesema mambo manne yanawatisha ndio hao viungo wanne wanaowatisha,” amesema Ahmed.