Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kinachoibeba Real Madrid kuiteka dunia

Real Madrid Uefaaaaaaaaaa Kinachoibeba Real Madrid kuiteka dunia

Fri, 26 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko la mamlaka na vyanzo mbalimbali vinavyotoa taarifa, kumbukumbu na takwimu zinazohusu michezo na hasa soka.

Mara nyingi vyanzo hivi hutofautiana linapokuja suala la kushindanisha klabu na hata mataifa hasa kuhusu ubora na mafanikio.

Hata hivyo, kuna mahali karibu vyanzo na asasi zote zinakubaliana na kama hazikubaliani basi zinakaribiana, na hapo ni kuhusu mafanikio, ubora na ukubwa wa klabu ya Real Madrid ya Hispania katika soka la Ulaya na dunia kwa jumla.

Hivi majuzi Real Madrid ilitangazwa ndiyo klabu ya soka yenye thamani kubwa zaidi duniani, Euro 6.6 bilioni (karibu Sh20 Trilioni).

Mapato ya mwaka 2023/24 ya Real Madrid yamefika zaidi ya Euro bilioni 1 (takriban Sh3 Trilioni) na hivyo kuwa klabu ya kwanza ya soka kufikia pato la zaidi ya Euro 1 bilioni.

Ni klabu yenye mafanikio makubwa sana Hispania na Ulaya kwa jumla na mapato na mafanikio hayo ya kifedha hayajatoka hewani, mafanikio yalileta kipato na kipato kuleta mafanikio.

Hata hivyo, nafasi ya Madrid katika dola ya Hispania ilichangia sana katika mafanikio na wengine wanasema pia ni kutokana na upendeleo kutoka familia ya kifalme ya taifa hilo na uliipa klabu hyo nafasi na masilahi tofauti na klabu nyingine.

Real Madrid au Los Blancos (Weupe) ilianzishwa Machi 6, 1902 na jina la Real (Royal) lina maana ya kifalme na walipewa rasmi na mfalme Alfonso wa 13 mwaka 1920. Hii ni klabu inayoongozwa na wanachama.

Madrid ni miongoni mwa klabu tatu zilizoanzisha Ligi ya Hispania na haijawahi kushuka tangu mwaka 1947, ikiweka rekodi ya kushinda ubingwa wa Hispania mara 36 na vikombe vingi vya ndani kama Copa De Roy na Supa Copa na ina rekodi ya kuchukua ubingwa mara 12 katika misimu 16.

Ndiyo imetawala soka la Hispania, kiasi kwamba wapinzani na watani zao FC Barcelona na Atletico Madrid wataendelea kuzimezea mate rekodi hizo kwa miongo na hata karne nyingi zijazo.

Imetawala pia soka la Ulaya hasa kuanzia miaka ya 1950 na 1960 na ilikuwa moto wa kuotea mbali na hadi sasa imenyakua makombe karibu katika kila mashindano ya Ulaya.

Weupe hao wa Madrid, imeweka rekodi katika msimu wa 2023/24 kwa kuchukua ubingwa wa 15 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ukiwa ni wao watano katika misimu tisa, pia imebeba Uefa Super Cup mara tano na Uefa Cup mara mbili.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Takwimu na Historia ya Soka (IFFHS), Real Madrid imeshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nyingi kuliko klabu nyingine ikiwa na rekodi ya kufunga mabao mengi, kushinda mechi nyingi na sare nyingi kuliko zote.

Inatambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kama klabu bora ya karne ya 20 na imenyakua ubingwa wa klabu duniani mara nane ikiwa ni rekodi pia katika mashindano hayo.

Mafanikio haya ni matokeo ya mipango mizuri na mafanikio yaliyotokana na mipango hiyo kiasi cha kuvutia mashabiki Hispania, Ulaya na duniani kwa jumla.

Pia ndio klabu yenye mashabiki wengi duniani na ina wafuasi wengi kuliko klabu yoyote katika mitandao ya kijamii na imekuwa na mipango mizuri ya kifedha na ya uwanjani hivyo uwekezaji wao mkubwa unaonekana katika matokeo makubwa uwanjani.

Moja ya mihamala iliyowaimarisha Madrid ilikuwa mauzo ya uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo kwa Halmashauri ya Jiji la Madrid yaliyowaingizia fedha zilizosaidia kulipa madeni ya klabu Euro 270 Milioni na kuwekeza katika kununua wachezaji ghali kama Cristiano Ronaldo.

Madrid ina falsafa ya kununua wachezaji nguli duniani au ‘Galacticos’ na Alfred Di Stefano ndiye anatajwa ni mchezaji wa kwanza kununuliwa ghali miaka ya 1950, kabla ya ujio wa kina Zinedine Zidane, Luis Figo, David Beckham, Ronaldo De Lima na wengineo na waliwatumia zaidi kibiashara na kuingiza pesa za kutosha.

Falsafa ya Galacticos iliendelea zaidi baada ya ujio wa Rais wa klabu hiyo, Florentino Perez na imekuwa ikiingiza wachezaji mmoja au wawili kwa msimu.

Ujio wa mchezaji nguli wa Paris Saint Germain na timu ya taifa ya Ufarasa, Kylian Mbape Madrid msimu huu ni mwendelezo wa utamaduni na falsafa hiyo.

Cristiano Ronaldo aliyefunga mabao 451 katika michezo 438 aliyoichezea klabu hiyo anabaki kuwa kielelezo cha mafanikio ya falsafa hiyo na atabaki kwenye kumbukumbu kama mchezaji wa klabu hiyo aliyefikia wastani wa kufunga bao moja au zaidi katika kila mchezo wa timu hito.

Christiano ameshinda taji la La Liga mara nne na ubingwa wa Ulaya mara nne akiwa kwenye nyumba nyeupe hiyo ya Madrid.

Ikiwa ni klabu ya wanachama, Madrid inaingiza fedha nyingi kupitia manunuzi ya bidhaa kama jezi, skafu, kofia na bidhaa nyingine.

Pia, timu hiyo inayotumia uwanja wa Santiago Bernabeu tangu mwaka 1947 imekuwa ikiingiza pato kubwa kutokana na viingilio vya mashabiki na watalii wanaofika katika viunga vya klabu hiyo.

Yote kwa yote, ni jambo lisilokuwa la kawaida litakaloweza kuwaondoa Madrid katika utawala wa dunia na kama hilo litatokea bado itachukua mamia kama si maelfu ya miaka kuiondoa nembo ya kifalme ya Madrid katika rekodi nyingi walizoziweka katika matukio na mafanikio mbalimbali duniani.

Chanzo: Mwanaspoti