Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kina Magoma, Yanga mahakamani tena leo, uamuzi utakavyokuwa

Kesi Ya Kina Magoma Dhidi Ya Yanga Kuendelea Leo Mahakamani.png Kina Magoma, Yanga mahakamani tena leo, uamuzi utakavyokuwa

Mon, 9 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hatima ya uhalali wa rufaa dhidi ya Klabu ya Dar es Salaam, Young African Sports, maarufu Yanga, inatarajiwa kujulikana leo Jumatatu, Septemba 9, 2024, wakati Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam, itakapotoa uamuzi wa pingamizi dhidi ya rufaa hiyo.

Rufaa hiyo imefunguliwa na Juma Ally Magoma na mwenzake Geoffrey Mwaipopo, wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu kuiongezea Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo na wenzake muda wa kufungua shauri la maombi ya marejeo.

Klabu hiyo iliomba kuongezewa muda huo ili kufungua shauri hilo la marejeo au hukumu ya mahakama hiyo iliyobatilisha Katiba yake ya sasa kufuatia kesi ya msingi iliyofunguliwa na Magoma na mwenzake, wakihoji uhalali wa katiba hiyo.

Magoma na Mwaipopo ambao wanaojitambulisha kama wanachama wa klabu hiyo, hawakukubaliana na uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu kuiongezea muda bodi hiyo ya Yanga kufungua shauri hilo la marejeo, hivyo wakakimbilia Mahakama Kuu ambako walikata rufaa hiyo.

Wajibu rufaa katika rufaa hiyo ni Bodi hiyo ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga (mjibu rufaa wa kwanza), Fatma Abeid Karume (mjumbe wa bodi hiyo mpaka sasa), Abeid Abeid na Jabiri Katundu, ambao pia waliwahi kuwa wajumbe wa bodi ya klabu hiyo.

Bodi ya wadhamini wa Yanga imewawekea pingamizi la hoja za kisheria kina Magoma dhidi ya rufaa hiyo, ikibainisha hoja mbili. Kwanza inadai uamuzi ambao kina Magoma wameukatia rufaa na ya pili wanadai rufaa hiyo imeshapitwa na tukio.

Uamuzi wa pingamizi hilo ambao ndio utakaoamua hatima ya uhalali wa rufaa hiyo umepangwa kutolewa leo Jumatatu na Jaji Mfawiidhi wa mahakama hiyo, Salma Maghimbi.

Pingamizi hilo lilisikilizwa Agosti 30, 2024, ambapo mawakili pande zote Kalaghe Rashid wa Yanga na Jacob Mashenene wa kina Magoma walichuana kwa hoja za kisheria kila mmoja akijitahidi kuishawishi mahakama ikubaliane nao na kurejea kesi mbalimbali kusisitiza hoja zao

Mahakama katika uamuzi wake itaamua iwapo hoja za pingamizi hilo la Yanga zina mashiko au la. Hivyo kama itakubaliana na pingamizi hilo basi rufaa hiyo ya kina Magoma itatupiliwa mbali.

Hata hivyo, kama mahakama katika uamuzi wake itatupilia mbali pingamizi la Yanga, sasa itaendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo na kisha kupanga tarehe ya uamuzi wa rufaa hiyo.

Chimbuko la rufaa hiyo ni kesi iliyofunguliwa na Magoma na Mwaipopo Agosti 4, 2022, wakipinga Katiba hiyo ya mwaka 2011 kuwa si halali kisheria na kwamba Katiba halali inayotambulika ni ile ya mwaka 1968.

Hivyo waliiomba mahakama hiyo itamke kuwa Katiba ya mwaka 2011 ni batili na wajumbe wa bodi waliopo kwa Katiba ya sasa hawana uhalali na miamala yote ya kifedha waliyoifanya ni batili.

Kesi hiyo ilisikilizwa na Hakimu Pamela Mazengo, upande mmoja bila wadaiwa wengine kuwepo isipokuwa Abeid pekee, kwa madai kuwa walipelekewa wito wa Mahakama lakini hawakuitikia.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake Agosti 2, 2023, ilikubaliana na hoja za kina Magoma, ikabatilisha Katiba ya sasa ya Yanga ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2011, kuwa haitambuliki kisheria na kwamba Katiba halali ya klabu hiyo ni ya mwaka 1968

Pia ilisema hivyo kuwa Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya mwaka 2011 si halali na chochote kilichofanywa na bodi hiyo ni batili na ikaamuru Bodi ya Wadhamini ya mwaka 1968 ndio irejeshwe katika uongozi kuendesha klabu hiyo.

Pia mahakama hiyo iliamuru kuwa miamala yote ya kifedha iliyofanywa na Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya sasa ni batil.

Wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa Yanga kwa sasa ni George Mkuchika (mwenyekiti ), Fatma Abeid Aman Karume, Dk Mwigulu Lameck Nchemba, Tarimba Abbas na Anthony Mavunde.

Hukumu hiyo iliibuka Julai 16, 2024, mwaka mmoja baadaye kupitia vyombo vya habari likiwemo Mwananchi, baada ya walalamikaji hao kurudi mahakamani kuomba utekelezaji wa hukumu hiyo.

Uongozi wa Klabu hiyo, kupitia Mkurugenzi wake wa Sheria, Wakili Simon Patrick ulieleza haukuwa unafahamu kuwepo kwa kesi na hukumu hiyo. Mpaka wakati huo ilipoupata uamuzi huo ilikuwa imeshachelewa kuchukua hatua zozote za kuupinga.

Hivyo ililazimika kuomba kuruhusiwa kufungua shauri la maombi ya marejeo kupinga hukumu hiyo nje ya muda, ikakubaliwa ndipo wakafungua maombi haya ya marejeo.

Kufuatia uamuzi huo ndipo kina Magoma wakakata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.

Hata hivyo Agosti 5, 2024, Mahakama ya Kisutu ilisikiliza shauri la maombi ya marejeo la Wadhamini wa Yanga na katika uamuzi wake ilioutoa Agosti 9, 2024, Mahakama hiyo ilikubaliaa na hoja za Yanga ikatengua hukumu yake ya awali iliyokuwa imebatilisha Katiba ya Yanga ya sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live