Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kina Kamungo wapo wengi, tatizo ni sheria tu

Kamungo Messiii.png Kina Kamungo wapo wengi, tatizo ni sheria tu

Mon, 16 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwaka 2012, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimruhusu kocha wa zamani wa timu ya taifa, Kim Poulsen kwenda Uingereza kwa mapumziko, lakini tulimwomba atumie ziara hiyo kusaka wachezaji kwa ajili ya timu ya taifa, na hasa Adam Nditi ambaye wakati huo alikuwa kinda.

Nditi alishachezea timu ya taifa ya England kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 21 na alikuwa moto kwenye klabu yake ya Chelsea, akicheza kama beki wa pembeni na wakati mwingine kiungo.

Poulsen alifanikiwa kukutana na Nditi, ambaye alienda Uingereza akiwa na miaka 18, alifanya mazungumzo ya kina na mchezaji huyo kuhusu kuwa tayari kulichezea taifa lake.

Nditi hakuwa na kikwazo kwake kuitikia wito huo, lakini akasema tatizo kubwa ni kwamba alishachukuwa uraia wa Uingereza kwa ajili ya kumrahisishia maisha, wakati klabu yake ikiwa katika safari za nje ya taifa hilo, ambalo wakati huo lilikuwa ndani ya Jumuiya ya Ulaya.

Alisema kuchukua uraia wa Uingereza haikuwa kikwazo, lakini kikwazo ni sheria za Tanzania zisizoruhusu uraia wa nchi mbili, maarufu kama uraia pacha.

Hii ni sheria ambayo imewezesha mataifa mengi ya Afrika, Asia na Amerika ya Kusini kunufaika na wachezaji waliokulia Ulaya na kupata mafunzo sahihi kuanzia utotoni.

Pia ndio sheria inayonufaisha mataifa makubwa kuweza kutumia wachezaji wenye vipaji wenye asili ya Afrika au Amerika Kusini, kama Kylian Mbappe, Karim Benzema kuchezea timu zao za taifa.

Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), mchezaji anaweza kuamua kuichezea timu ya taifa ya nchi nyingine, hata kama hapo awali aliitwa na kuichezea timu ya taifa lake la sasa ya mashindano yanayozingatia umri.

Tumeona baba yake Mbappe alitamani mwanae aichezee Cameroon, lakini ubabaishaji wa viongozi wa soka wa taifa hilo ulimrudisha nyuma na tangu hapo nyota huyo wa Paris Saint Germain hataki kuisikia Cameroon.

Yupo nyota wa zamani wa Ivory Coast na klabu ya Chelsea, Solomon Kalou, ambaye Uholanzi ilitaka aichezee timu yake ya taifa na alishaitwa kwenye timu za vijana, lakini akaamua kuichezea Ivory Coast.

Lakini Kelvin Prince Boateng, akiwa Hertha Berlin, aliwaambia waandishi wa habari mazoezini jijini Berlin kuwa hangekubali wito wa kuichezea Ghana, akisema Ujerumani ilihangaika kumkuza kisoka na kumpa kila alichotaka hadi kufikia kuwa mchezaji nyota, bila ya Ghana kusumbuka kwa lolote.

Alishangaa Ghana imeamua kumuita baada ya kuona imefuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Ujerumani wakati huo.

Hata hivyo, baada ya mazungumzo ya kina, winga huyo akaamua kuichezea Ghana, huku kaka yake Jerome Boateng akiichezea Ujerumani; ndugu wawili wa tumbo moja wakichezea mataifa mawili.

Mjadala wa wachezaji Watanzania walio nje umeibuka tena wakati huu baada ya nyota chipukizi, Bernard Kamungo kuitwa katika kikosi cha awali cha Olimpiki cha taifa la Marekani.

Kamungo alishindwa kuichezea Tanzania awali kutokana na tatizo la hati ya kusafiria.

Hata kama leo serikali ya Tanzania itaamua kushughulikia hati hiyo muhimu ili aje kuichezea Taifa Stars, bado kutabakia kikwazo cha kutokuwepo kwa sheria ya uraia pacha.

Ni ama Kamungo akubali kuukana uraia wa sasa wa Marekani, kwa kuwa kwa kuichezea timu ya Olimpiki ni lazima atakuwa ameshapewa hati hiyo ya kusafiria, ama Tanzania ikubali haraka kuruhusu uraia wa nchi mbili, utakaomwezesha mchezaji huyo kuendelea na uraia wa Marekani, huku akichezea Tanzania.

Kwa hiyo, hadi sasa alipo, Kamungo anaweza wakati wowote kuiacha Marekani na kuichezea Tanzania, lakini sina uhakika kama atakuwa tayari kuukana uraia wa Marekani ili apate wa Tanzania kwa ajili ya soka labda kama hakutakuwa na usumbufu kama wapatao wachezaji kutoka nje ya Jumuiya ya Ulaya wanaochezea klabu za eneo hilo.

Naamini si Kamungo pekee anayekabiliwa na kikwazo hicho. Naamini wapo wachezaji wengi walioenda Ulaya au Marekani wakiwa bado kinda na sasa wanaanza kuimarika kama wachezaji wa kulipwa na inawezekana kabisa wana nia hiyo, lakini kutokana na kujijenga kwenye nchi hizo, wanaona vigumu kuachana na uraia wa sasa kwa ajili ya kuichezea Tanzania.

Pale, TFF kila mara kuna maombi yanakuja ya wachezaji vijana na wazee kwenda kusakata soka nje, lakini wengi wao hawamo kwenye mitandao ya wajanja wa mjini na hivyo kupotea.

Kitu kinachoweza kuwafanya wajitokeze ni mafanikio makubwa ambayo Taifa Stars inaweza kupata, kama ilivyokuwa kwa Ghana, au kupata kocha ambaye ataamua kutumia muda wake mwingi kusaka wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaosakata soka nje ya nchi bila ya kujali wako klabu za daraja gani, kama alivyofanya yule kocha wa Comoro au Madagascar.

Suala la uraia pacha limekuwa likiibuka kila mara, hasa kwa wale waliohamia nchi za Ulaya au Marekani, lakini bado halijawahi kuwa na mjadala mkubwa uliosababisha hatua kuchukuliwa na kulipatia ufumbuzi.

Kwa upande wa soka huwa suala hilo halizungumzwi kwa kina kwa sababu idadi ya wanasoka wenye asili ya Tanzania wanaong’ara nje ni ndogo na huibuka wakati fulani na kupotea.

Ni muhimu suala hili la uraia pacha sasa likaangaliwa kwa mapana na marefu yake ili ijulikane kwamba linawezekana au haliwezekani ili nguvu zielekezwe sehemu nyingine. La sivyo litakuwa likimalizwa kwa ahadi zisizotimia, lakini zenye uwezo wa kuibuka kila mara, kutikisa na baadaye kutoweka.

Lililo wazi ni kwamba kina Bernard Kamungo wako wengi, lakini tatizo na sheria itakayoondoa kikwazo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live